1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Idadi ya watu China yapungua kwa mara ya kwanza

17 Januari 2023

Kwa mara ya kwanza katika muda wa miongo sita, data zimeonyesha kuwa idadi ya watu nchini China imepungua. Wachambuzi wanaonya hali hii inaweza kukwamisha ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo ya Asia

https://p.dw.com/p/4MILm
China | Bevölkerungswachstum
Picha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Taifa hilo lenye wakaazi zaidi ya bilioni moja na milioni mia nne linashuhudia kuporomoka kwa viwango vya watoto wanaozaliwa, wakati huo huo idadi kubwa ya watu wazima ikiingia katika umri wa kustaafu.

Wachambuzi wanaonya kuwa hali hii inaweza kukwamisha ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo ya Asia na kuongeza shinikizo kwenye pato lake la kitaifa. Takwimu zilizochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu imeonyesha kuwa idadi ya watu wa China bara mwaka 2022 ni pungufu ya watu 850,000 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Katika kipindi hicho cha mwaka mmoja, walikufa watu milioni 10.41, huku watoto waliozaliwa wakiwa milioni 9.56. China imeifuta sera yake ya miaka ya 1980 ya mtoto mmoja kwa kila familia iliyowekwa kuondoa kitisho cha idadi ya watu kubwa kupindukia.