1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaPakistan

Idadi ya waliouwawa kwa bomu Pakistan yafikia 57

29 Septemba 2023

Takriban watu 57 wamekufa na wengine zaidi ya 70 wamejeruhiwa hii leo nchini Pakistan, kufuatia shambulio la kujitoa mhanga wakati wa sherehe za kidini huko Mastung katika mkoa wa kusini magharibi wa Baluchista.

https://p.dw.com/p/4WyoY
Majeruhi wakipatiwa matibabu
Majeruhi wa bomu la kujitoa mhanga wakiwa wamelazwa hospitali Picha: District Police Office/AP Photo/picture alliance

Shambulio lilitokea wakati waumini wapatao 500 wa Kiislamu walipokuwa wakisherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad, katika sherehe zinazofahamika kama Maulid an-Nabii.

Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi eneo hilo Munir Ahmed ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa mshambuliaji alijilipua karibu na gari la Naibu Msimamizi wa jeshi la Polisi lililokuwa limeegesha karibu na msikiti uliobomoka na kuwafukia chini ya vifusi watu wengine kati ya 30 na 40.

Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na mlipuko huo ambao inajiri huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya makundi ya wapiganaji magharibi mwa Pakistan, hali inayozidisha changamoto kwa vikosi vya usalama kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Januari mwakani.