1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wahamiaji waliokufa baharini yazidi 110

Admin.WagnerD4 Oktoba 2013

Waokoaji nchini Italia wanakabiliana na hali mbaya ya hewa baharini katika juhudi za kutafuta miili ya wahamiaji waliozama baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupata ajali. Idadi ya waliothibitishwa kufa imefika 111.

https://p.dw.com/p/19teA
Maiti za wahamiaji zilizoopolewa kutoka baharini
Maiti za wahamiaji zilizoopolewa kutoka bahariniPicha: picture-alliance/dpa

Mawimbi makubwa yanawatatiza wapiga mbizi wanaojaribu kuifikia boti iliyokuwa na wahamiaji kutoka Afrika, ambayo ilizama jana asubuhi karibu na kisiwa cha Lampedusa nchini Italia. Mpigambizi wa kwanza aliyeweza kuikaribia boti hiyo ambayo imezama katika kina cha mita 47 Rocco Canell amesema imejaa miili ya watu waliokufa, na kuifananisha aliyoyaona na filamu ya kutisha.

Maiti za waliokufa katika ajali hiyo zimejaa kwenye hangari katika uwanja wa ndege, wakati majeneza ya kuzihifadhi yakisafirishwa kutoka mjini Sicily. Miongoni mwa waliokufa ni watoto na akina mama wajawazito, kama anavyoeleza Angelino Alfano, waziri wa mambo ya ndani wa Italia ambaye alizuru kisiwa cha Lampedusa baada ya ajali.

Maiti zaidi zinazidi kuwasilishwa kutoka baharini
Maiti zaidi zinazidi kuwasilishwa kutoka bahariniPicha: picture-alliance/dpa

''Nimeona maiti 93 zikiwa katika mifuko maalum ya kuzihifadhia. Maiti nne ni za watoto, na mbili ni za wanawake wajawazito. Wamo wanaume na wanawake, na nimeshuhudia maiti zingine kumi zikiwasilishwa kutoka baharini. Inasikitisha kwamba maiti zaidi zitapatikana, leo na kesho'' Amesema waziri Alfano.

Italia yaomboleza

Italia imeitangaza Ijumaa ya leo kuwa siku ya maombolezi ya kitaifa kwa watu hao walioangamia baharini. Bendera katika majengo ya serikali zinapepea nusu mlingoti, na watoto mashuleni wamenyamaza kimya kwa dakika moja kuwakumbuka wahanga.

Maduka mengi katika kisiwa cha Lampedusa yamefunga. Kiongozi wa Kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis amesema leo ni siku ya kilio.Inaaminika kuwa wengi wa watu waliokuwa ndani ya boti hiyo iliyozama ni raia wa Eritrea na Somalia.

Idadi ya waliokufa yatazamiwa kupanda

Watu 155 kati ya 500 ambao inakadiriwa walikuwa ndani ya boti hiyo ndio walionusurika kifo. Kwa ujumla inadhaniwa kuwa watu 300 walifariki katika ajali hiyo ambayo ni mojawapo ya mbaya kabisa kutokea katika mzozo wa wahamiaji wanaotaka kwenda Ulaya, kwa kipindi cha muongo mzima.

Wahamiaji husafiri katika mazingira yenye hatari kubwa baharini
Wahamiaji husafiri katika mazingira yenye hatari kubwa bahariniPicha: picture-alliance/Milestone Media

Ajali hiyo ilisababishwa na mkanyagano uliotokea ndani ya boti hiyo baada ya kifaa cha kubebea mafuta kushika moto, na kuwafanya watu wengi kukimbilia upande mmoja wa boti. Ilikuwa umbali wa km moja kutoka mwambao wa kisiwa cha Lampedusa. Baharia mmoja raia wa Tunisia amekamatwa na vyombo vya usalama vinavyochunguza ajali hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPAE/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman