1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo vya corona kuongezeka barani Ulaya

Saleh Mwanamilongo
30 Agosti 2021

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limeonya kuhusu uwezekano wa ongezeko la vifo barani Ulaya kutokana na covid-19,huku kampeni ya chanjo ikianza kusuasua.

https://p.dw.com/p/3zgzT
Albanien WHO Unterstützung Coronakrise Dr. Hans Kluge
Picha: Albania Ministry of Health and Social Protection

Tahadhari hiyo ya WHO imetolewa wakati idadi ya vifo kutokana na ugonjwa wa Covid-19 imepindukia watu milioni 4.5 kote duniani tangu kuanza kwa janga hilo.

Idadi ya maambukizi inazidi kuongezeka ulimwenguni kote, kufuatia kirusi cha aina ya Delta, hasa kwa watu ambao hawajapewa chanjo, huku hatua za kupambana na corona zikilegezwa.

Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO, barani Ulaya, Hans Kluge amesema maambukizo na vifo vimeongezeka tena hapa Ulaya, haswa katika mataifa masikini katika Balkans, Caucasus na Asia ya Kati.

"Nchi kadhaa zinaanza kuona udhia huu kuongezeka kwenye hospitali na pia vifo zaidi. Wiki iliyopita kulikuwa na ongezeko la asilimia 11 ya idadi ya vifo katika bara hili, na makadirio ya kuaminika yalitarajia vifo 236,000 hapa Ulaya ifikapo Desemba 1.",alisema Kluge.

Mashirika ya WHO na UNICEF yamezihimiza nchi za Ulaya kuwafanya waalimu kuwa miongoni mwa makundi yatakayopewa kipaumbele cha chanjo ili shule ziweze kukaa wazi baada ya mapumziko ya msimu wa joto.

Ufaransa kutoa chanjo milioni 10 za Covid-19 kwa afrika

Chanjo hizo zitatengwa na kusambazwa kupitia mfumo wa Umoja wa Afrika
Chanjo hizo zitatengwa na kusambazwa kupitia mfumo wa Umoja wa AfrikaPicha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Wakati hayo yanaarifiwa, Bara la Afrika litapokea jumla ya dozi milioni 10 za chanjo za AstraZeneca na Pfizer kutoka Ufaransa katika kipindi cha miezi mitatu ijayo. Rais Emmanuel Macron amesema hayo leo Jumatatu. Mwishoni mwa wiki iliopita Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel pia alitangaza msaada wa zaidi ya dozi milioni 70 ya chanjo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu kwa nchi masikini.

Hii leo, maalfu ya watu wanaopinga chanjo za corona wameandamana kwenye miji miwili ya Ugiriki wakilalamika kwamba masharti ya kuzuia corona ni magumu. Pamoja na masharti yaliyotangazwa na serikali ni kutowaruhusu watu kuingia kwenye mikahawa bila ya kuchanjwa.

India imefikia dozi milioni 10 ya chanjo kwa siku, huku idadi ya uzalishaji chanjo ikizidishwa mara mbili zaidi toka mwezi Aprili.

Watu zaidi ya elfu kumi wanakufa kila siku kutokana na Covid-19 kote ulimwenguni, idadi hiyo ikiwa ya chini ukilinganisha na kipindi kama hicho mwezi Januari Januari ambapo watu 15,000 walikuwa wanakufa kwa siku. Hata hivyo shirika la afya ulimwenguni limesema bado ni idadi kubwa ukilinganisha na ile ya mwanzoni mwa July ambayo ilikuwa chini ya vifo elfu saba kwa siku.