1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Idadi ya vifo Hanang yaongezeka na kufikia 89

Deo Kaji Makomba
12 Desemba 2023

Idadi ya vifo vilivyotokana na maporomoko ya matope, mawe na magogo kutoka katika mlima Hanang mkoani Manyara kaskazini mwa Tanzania imeongezeka na kufikia 89.

https://p.dw.com/p/4a5Uh
Tanzania | Watu wakibeba majeneza yaliohifadhi miili ya waliofariki kutokana na maporomoko ya matope wilayani Hanang
Watu wakibeba majeneza yaliohifadhi miili ya waliofariki kutokana na maporomoko ya matope wilayani Hanang TanzaniaPicha: Tanzania’s Ministry of Interior

Kulingana na taarifa iliyotolewa na kwa vyombo vya habari Jumatatu jioni Desemba 11 mwaka huu wa 2023, na msemaji mkuu wa serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi, imeeleza kuwa hadi sasa miili 87 imeishatambuliwa na ndugu zao kwa ajili ya mazishi huku miili mingine miwili ikiwa bado haijatambuliwa.

Maporomoko hayo yalitokea alfajiri ya Desemba 3 mwaka 2023 na kusababisha majeruhi 139 na kati yao 120 wamekwisharuhusiwa na waliobaki hospitalini ni 17.

Soma pia:Watu 65 wamefarki na 116 Majeruhi Tanzania

Wakati hayo yakitokea wananchi wilayani Hanang wametaka misaada inayotolewa na taasisi na jumuiya za watu mbalimbali kwa ajili ya watu walioathiriwa na mkasa huo, iwafikie walengwa na sio baadhi ya watu kujinufaisha binafsi.

Tayari Rais wa nchi hiyo Samia Suluhu Hassan amewaonya wanakamati wanaohudumia waathirika wa mkasa huo kuwa fedha za majanga sio fedha za kumnufaisha mtu binafsina kuwataka kuwa waadilifu katika matumizi ya fedha hizo.