1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA: Iran yazidisha urutubishaji urani hadi asilimia 60

18 Agosti 2021

Shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti silaha za atomiki IAEA limesema Iran imezidisha urutubishaji wa madini ya urani na kukaribia viwango vya kuunda silaha.

https://p.dw.com/p/3z846
Iran Urananreicherungsanlage in Natanz
Picha: AEOI/ZUMA Wire/imago images

Hatua hiyo inazidisha mvutano kati ya nchi za Magharibi na taifa hilo mnamo wakati pande hizo mbili zinataka kurudi kwenye mazungumzo ya kufufua mkataba wa kimataifa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. 

Kulingana na ripoti ambayo shirika la habari la Reuters limeona, Iran ilizidisha urutubishaji madini ya urani kutoka 20% hadi 60% mwezi Aprili, kama jibu la shambulizi lililopelekea usitishaji wa kazi katika kinu chake kilichoko Natanz. Matukio hayo yaliharibu kituo chake cha Natanz. Iran iliishutumu Israel kuhusika na shambulizi hilo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amethibitisha ripoti hiyo. Amesema kama ambavyo imesisitizwa mara kwa mara, hili ni jibu letu kwa kutotekelezwa kwa makubaliano ya Vienna pamoja na vikwazo vya Marekani.

Juhudi za kurejesha mazungumzo kati ya Iran na nchi za magharibi ya kufufua mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na pia kuirudisha Marekani kwenye mkataba huo unaendelea.
Juhudi za kurejesha mazungumzo kati ya Iran na nchi za magharibi ya kufufua mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na pia kuirudisha Marekani kwenye mkataba huo unaendelea.Picha: Lisa Leutner/AP Photo/picture alliance

Viwango vya urutubishaji madini ya urani vya silaha ni 90%. Mnamo mwezi Mei, shirika la Umoja wa Mataifa linalodhibiti matumizi ya nishati ya atomiki IAEA, liliripoti kwamba Iran ilikuwa ikitumia muundo ulioboreshwa wa urutubishaji hadi asilimia 60 ya madini ya urani katika kituo chake kilichoko Natanz. IAEA iliwaambia wanachama wake kwamba Iran inatumia nguzo ya daraja la pili kwa lengo hilo pia.

IAEA yataka majibu kutoka Iran kuhusu shughuli za nyuklia

Hatua hiyo ni miongoni mwa visa vya hivi karibuni vya ukiukaji wa vikwazo vilivyowekwa kufuatia mkataba wa mwaka 2015 kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Marekani na washirika wake kutoka Ulaya wameonya kwamba hatua kama hizo zinatishia juhudi za kufufua mazungumzoambayo yameahirishwa kwa sasa kuhusu mkataba huo.

Makao makuu ya shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya atomiki IAEA mjini Vienna, Austria.
Makao makuu ya shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya atomiki IAEA mjini Vienna, Austria.Picha: Michael Gruber/Getty Images

Kufuatia ripoti ya shirika la habari la Reuters kuhusu matukio hayo, Iran imesisitiza kuwa mpango wake kuhusu nyuklia ni salama na kwamba iliiarifu IAEA kuhusu urutubishaji wake. Imeongeza kuwa itabadilisha mienendo yake inayokinzana na mkataba wa 2015, ikiwa tu Marekani itarudi kwenye mkataba huo na iondoe vikwazo dhidi yake. Hayo yameripotiwa na shirika la habari linalomilikwa na serikali ya Iran.

Iran yasema itaanza kurutubisha madini ya Urani hatua inayakosolewa vikali

Mnamo Jumatatu, IAEA ilisema Iran imepiga hatua katika kurutubisha chuma cha urani, licha ya pingamizi kutoka nchi za magharibi kwamba hakuna matumizi ya kawaida na kuaminika kwa kazi kama hiyo.

Chuma cha urani huweza kutumiwa kutengeneza msingi wa bomu la nyuklia, lakini Iran inasema malengo yake ni ya amani na inalenga kutengeneza mtambo wa kuzalisha nishati

(RTRE;DPAE)