1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Human Rights Watch yalaani ukandamizaji nchini Rwanda

Saleh Mwanamilongo
17 Machi 2022

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema viongozi wa upinzani na wachambuzi nchini Rwanda, wanakamatwa na kufunguliwa mashataka kwa kutoa mitazamo yao ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/48cL3
Feierlichkeiten zum Tag der Streitkräfte in Mosambik
Picha: Estácio Valoi/DW

Katika ripoti yake iliyochapishwa jana Jumatano, Human Rights Watch inasema, imechunguza mashtaka na maamuzi ya majaji dhidi ya raia kadhaa wa Rwanda ambao wamekuwa wakitoa maoni ya kuikosoa serikali.

Mkuu wa Human Rights Watch katika kanda ya Afrika ya Kati, Lewis Mudge, amesema ni vigumu sana kwa watu nchini Rwanda, kutoa maoni yanayoikosoa serikali.

''Mfano mmoja,ni ule wa Kizito Mihigo, aliekamatwa na kutupwa jela bada ya kuimba wimbo ambao walionyesha mshikamano na wahanga wa uhalifu wowote,nchini Rwanda wimbo huo ulichukuliwa kama mstari mwekundu.''

Shirika la Human rights watch limesema kumekuwepo na sheria ambazo zinaminya uhuru wa kujieleza katika taifa hilo, hasa kwa wanasiasa na wachambuzi wanaotoa maoni yao kupitia mtandao wa Youtube.

Shirika hilo limesema limefanikiwa kuwahoji baadhi ya wanahabari walioshtakiwa pamoja na wanasiasa 11 wa upinzani waliokamatwa kwa kutoa mitazamo yao.

Soma piaMwanamuziki mashuhuri Rwanda Kizito Mihigo ajinyonga

''Watu hao wanatakiwa kuachiwa huru haraka''

Kizito Mihigo mwanamuziki mashuhuri ambaye polisi ilisema alijinyonga akiwa rumande
Kizito Mihigo mwanamuziki mashuhuri ambaye polisi ilisema alijinyonga akiwa rumandePicha: Getty Images/C. Ndegeya

Ripoti ya Human Rights Watch, imemnukuu mmoja wa watumiaji wa Youtube Dieudonne Niyonsenga maarufu kwa jina la Cyuma Hassan ambaye amefuguliwa mashtaka mahakamani, baada ya kuzungumzia visa vya haki za binadamu na ufisadi nchini humo na mwaka uliopita, alihukumiwa jela miaka saba.

Lewis Mudje amesema uhuru wa majaji nchini Rwanda upo mashakani na nilazima baadhi ya sheria nchini humo zirekebishwe.

''Kwetu sisi viongozi wa kishiria nchini Rwanda hawana uhuru wa kuhakikisha haki ya kutoa maoni imeheshimiwa kulingana na sheria ya kimataifa. Tumeshuhudia watu wanaohukumiwa kwa sababu ya kutoa maoni yao. Watu hao wanatakiwa kuachiwa huru haraka na bila masharti yoyote.''

Soma pia→Mwanamuziki mwingine maarufu afariki jela nchini Rwanda

Mnamo Machi 3, Human Rights Watch imesema ilimwandikia barua Waziri wa Sheria Emmanuel Ugirashebuja ili kutoa maoni kuhusu uchunguzi wake na kuomba taarifa kuhusu hatua za mamlaka ya Rwanda kushughulikia ukiukaji wa haki ya uhuru wa kujieleza. Lakini Serikali haijajibu.

Shirika la Human Rights watch limesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua msimamo na kushinikiza mamlaka kusitisha unyanyasaji,na kufuta mashtaka yote yanayowakabili wanachama wa upinzani,watumiaji wa YouTube na waandishi wa habari.