1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Hujuma za Urusi nchini Ukraine zasababisha vifo na majeruhi

8 Septemba 2023

Makombora ya vikosi vya Urusi yamewaua watu kadhaa na kuwajeruhi makumi wengine katika mashambulizi yaliyoyalenga maeneo mbalimbali nchini Ukraine usiku wa kuamkia Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4W6sZ
Ukraine Krieg l Nach einem russischen Angriff in Kryvyi Rih
Shambulizi la Urusi kwenye mji wa Kryvyi Rih (Rig) nchini Ukraine limesababisha vifo na majeruhi kadhaa.Picha: National Police of Ukraine/AP/picture alliance

Hujuma za ndege za kivita za Urusi ndiyo zimehusika pakubwa kwa mashambulizi yaliyowauwa watu kadhaa nchini Ukraine.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine, Ihor Klymenko, amesema watu watatu wameuwawa na wengine wanne wamejeruhiwa baada ya kombora la Urusi kukilenga kijiji kimoja kwenye jimbo la Kusini mwa Ukraine la Kherson hii leo.

Taarifa hizo zimetolewa na waziri huyo kupitia mtandao wa Telegram akisema kijiji kilicholengwa kinaitwa Odradokamianka.

Kwenye wilaya nyingine ya Kryvyi Rig, makombora kadhaa ya Urusi yalililenga jengo la utawala na kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine wawili.

Wilaya hiyo inapatikana kwenye mkoa wa kusini mashariki mwa Ukraine wa Dnipropetrovsk na ndiyo mji wa nyumbani kwa rais wa Ukraine Volodomyr Zelensky.

Mashambulizi ya Urusi yanavurumishwa kila kona ya Ukraine

Kaskazini mwa Ukraine karibu na mpaka na Urusi kombora limeharibu nyumba 20, magari 8 na kuwajeruhiwa watu wawili.

Kulikuwa na kombora jingine lililorushwa kusini mwa nchi hiyo karibu na mkoa wa Zaporizhzhya ambalo limejeruhi mtu mmoja.

Kwa jumla vikosi vya Moscow vinavurumisha makombora kila kona ya Ukraine wakati vinajaribu kuwazidi nguvu wapiganaji wa taifa hilo.

Vikosi vya Ukraine navyo vimekuwa vikifanya mashambulizi ya hapa na pale vikilenga kujibu mapigo na kuleta hasara upande wa Urusi.

Ukraine Krieg l Nach einem russischen Angriff in Kryvyi Rih
Juhudi za uokoaji zikiendelea katika moja ya maeneo yaliyolengwa na Urusi huko Ukraine.Picha: Ukrainian Emergency Service/AP/picture alliance

Inaarifiwa vilevile vikosi vya Kyiv vinasonga mbele upande wa kusini eneo ambalo limekuwa uwanja wa mapambano makali baina yapande hio mbili.

Ukraine ikijibu mapigo kwa dhamira ya kuyakomboa maeneo yaliyotwaliwa na Urusi, huku Moscow inatumia kila mbinu kuzima nguvu ya vikosi vya Kyiv kusonga mbele.

Ukraine imekuwa vilevile ikipanga hujuma dhidi ya miundombinu ya Urusi, vikosi vyake vikishukiwa kutumia zaidi droni kuingia ndani ya ardhi ya Urusi.

Mathalani mapema leo, Moscow ilisema  mifumo yake ya ulinzi ilidungua ndege moja isiyo na rubani iliyolilenga eneo la kaskazini mwa rais ya Crimea ambayo Urusi iliinyakua kwa mabavu mwaka 2014.

Urusi yaendesha chaguzi maeneo ya Ukraine inayoyadhibiti

Ukraine Krieg l Kommunalwahlen in der russisch kontrollierten Region Donezk l Stimmabgabe
Uchaguzi ukiendelea kwenye majimbo ya Ukraine yanayodhibitiwa na Urusi Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Wakati mapigano hayaoneshi dalili ya kupungua makali, mamlaka za Urusi zinaendesha uchaguzi wa ngazi ya wilaya na mitaa kwenye maeneo ya Ukraine inayoyadhibiti.

Lengo ni kutanua usimamizi wa Moscow kwenye maeneo hayo kwa kuwezesha kuchaguliwa wanasiasa watakaotekeleza sera za Urusi.

Uchaguzi huo kwenye majimbo ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia umeanza leo na utaendelea hadi siku ya Jumapili. Tayari zoezi hilo limekosoelwa vikali na serikali kuu mjini Kyiv na washirika wake wa magharibi.

Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya limeutaja uchaguzi huo kuwa ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa.

Serikali ya Ukraine nayo imesema uchaguzi huo unatishia usalama wa raia wa Ukraine kwenye maeneo hayo na imeitaka Jumuiya ya Kimataifa kutoyatambua matokeo yake.