1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Huenda ligi ya kandanda Ujerumani ikaanza tena ila...

22 Aprili 2020

Mashirika ya soka hapa Ujerumani yamekiri kuwa hayawezi kuhakikisha usalama wa asilimia 100 wa kiafya kwa kila mtu lakini yako tayari kuchukua hatua za tahadhari ili ligi kuanza tena mwezi ujao.

https://p.dw.com/p/3bGKi
Fußball Bundesliga Marco Reus und Erling Haaland
Picha: Imago Images/Team 2

Haya ni kwa mujibu wa gazeti la Suddeutsche.

Gazeti hilo limesema limepata nyaraka zilizokusanywa na jopokazi la kitengo cha ligi kinachopanga ratiba za mechi, DFL na shirikisho la soka la Ujerumani, DFB zinazoeleza hatua ambazo zitachukuliwa ili kuruhusu mechi kuchezwa bila ya kuwepo mashabiki.

Jopokazi hilo linaloongozwa na mkuu wa kamati ya kitabibu ya DFB Tim Meyer limesema timu nzima haitolazimika kwenda karantini iwapo mchezaji mmoja atapatikana kuwa na virusi vya Corona. Iwapo mchezaji ataambukizwa, basi anapaswa kutengwa na kufanyiwa vipimo.

Vile vile, nyaraka hizo zinaeleza sheria za usafi ambazo zinapaswa kuzingatiwa na timu ikiwemo hoteli wanakolala, vipimo na ufwatiliaji wa afya za wachezaji.

Nalo gazeti la michezo la Kicker limesema jopokazi hilo limeweka kanuni ambazo zinaruhusu timu kuanza tena mazoezi. Wachezaji watakuwa wanafanya mazoezi japo kwa vikundi vidogo vidogo. Nyaraka hizo zitawasilishwa kwa wanachama wa DFL mnamo siku ya Alhamisi.

Ligi kuu ya Bundesliga ambayo ilikuwa imesalia na mizungunko tisa kukamilika, inatarajiwa kuanza tena mnamo mwezi Mei.