1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Wahanga wa ukatili wa kijinsia wakosa msaada Kenya

21 Septemba 2021

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Human Rights Watch limeikosoa serikali ya Kenya kwa jinsi ilivyoshughulikia visa vya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa janga la Covid-19.

https://p.dw.com/p/40bLc
Nigeria Protest Vergewaltigung
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Alamba

Katika ripoti yake, Human Rights Watch imesema visa vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana viliongezeka maradufu wakati serikali ya Kenya ilipoweka vizuizi vya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona. 

Ripoti yenye kurasa 61 iliyotolewa leo na kupewa jina "Sikuwa na mahali pa kwenda," imeainisha kasoro za serikali ya Kenya katika kuzuia visa vya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa janga la Covid-19.

Ripoti hiyo ya Human Rights Watch inaendelea kueleza kuwa kujikokota kwa serikali katika kutoa msaada kwa wahanga kulichangia kwa visa vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kuongezeka maradufu.

Soma pia: HRW yashutumu unyanyasaji wa mashirika ya kiraia Uganda

Wahanga walikabiliwa na uwezekano wa kudhurika hata zaidi kutokana na kushindwa kwa serikali kuhakikisha wanapata matibabu bora na kwa wakati, msaada wa kifedha na pia kuchunguza visa hivyo vya unyanyasaji ili waathiriwa wapate haki.

Mtafiti mwandamizi wa shirika la Human Rights Watch ambaye pia anasimamia ofisi ya shirika hilo mjini Nairobi, Agnes Odhiambo amesema, "Janga la Covid-19 sio la kwanza nchini Kenya kushuhudia ongezeko la visa vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana. Serikali ilipaswa kuwa tayari kushughulikia visa hivyo, lakini kama ilivyokuwa awali, serikali imelifumbia macho suala hilo na kushindwa kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya unyanyasaji."

Wanawake wanaoishi katika umaskini wameathirika zaidi wakati wa janga la Corona

Südafrika Protest gegen Frauengewalt
Wanawake wakiandamana kupinga visa vya ukatili dhidi ya waoPicha: Reuters/S. Hisham

Human Rights Watch iliwahoji wahanga kumi na mbili wa unyanyasaji wa kijinsia, wakiwemo wazazi wanne na jamaa wa wasichana waliodhulumiwa kimapenzi, idara ya serikali inayosimamia masuala ya kijinsia miongoni mwa wengine.

Kenya, kama ilivyokuwa kwa nchi nyengine duniani, ilishuhudia ongezeko la visa vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana wakati serikali ilipoweka vizuizi ili kupambana na kuenea kwa virusi vya corona. Hata kabla ya kuanza kwa janga la corona, visa vya unyanyasaji na dhulma za kingono bado vilikuwa tatizo kubwa nchini Kenya.

Soma pia: HRW: Serikali za Afrika ziwekeze kwenye elimu ya watoto

Wahanga waliohojiwa wameelezea kupigwa, ndoa za utotoni, dhulma za kingono na ukeketaji huku wasichana na wanawake wanaoishi katika lindi la umaskini wakiathirika zaidi wakati wa janga la corona.

Human Rights Watch imesema wengi waliokuwa wakifanya hujuma hizo ni jamaa wa karibu au hata familia.

Hata hivyo, wahanga wengi hawakuripoti unyanyasaji huo kwa mamlaka kwa sababu hawakuamini kuwa watapata msaada, wakati wengine wakihofia kuwa watalazimika kutoa rushwa ili kesi zao zishughulikiwe.