HRW imesema wahamiaji wauwawa Saudi Arabia
21 Agosti 2023Wahamiaji hao waliokuwa wakivuka mpaka kuingia nchi hiyo kupitia Yemen. Kwa mujibu wa ripoti ya Human Rights Watch iliyochapishwa leo Jumatatu, walinzi wa Kisaudi, waliwamiminia risasi kama mvua, wahamiaji wa Kiethiopia waliokuwa wakijaribu kuingia Saudi Arabia. Duru kutoka serikali ya Saudi Arabia imeiita ripoti hiyo ni madai yasiyokuwa na msingi. Hata hivyo, shirika hilo lenye makao yake jijini New York ambalo limekuwa likiorodhesha matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya wahamiaji wa Kiethiopia ndani ya Saudi Arabia na Yemen kwa takribani mwongo mmoja, limesema mauaji haya ya hivi karibuni yanaonesha kusambaa na kutekelezwa kwa mpangilio maalum na huenda yakafikia viwango vya kuitwa uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mwaka jana wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliripoti juu ya kuwwepo madai yakutia wasiwasi kuhusu mashambulio ya makombora na silaha ndogo ndogo yaliyofanywa na walinda usalama wa Saudi Arabia na kuua takriban wahamiaji 430 kusini mwa nchi hiyo na Kaskazini mwa Yemen.