1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Saudi Arabia iliwashambulia wahamiaji wa Ethiopia

21 Agosti 2023

Shirika la Human Rights Watch limetoa ripoti mpya Jumatatu inayoituhumu Saudi Arabia kwamba iliwafyatulia makombora wahamiaji wa Ethiopia waliokuwa wakijaribu kuingia nchi hiyo wakitokea Yemen.

https://p.dw.com/p/4VOnw
Wahamiaji wa Ethiopia wakishuka kwenye boti pwani ya Ras al-Ara, Lahj Yemen, kwa lengo la kufika Saudi Arabia. (Picha ya maktaba Julai 26, 2029)
Wahamiaji wa Ethiopia wakishuka kwenye boti pwani ya Ras al-Ara, Lahj Yemen, kwa lengo la kufika Saudi Arabia. (Picha ya maktaba Julai 26, 2029)Picha: Nariman El-Mofty/AP/picture alliance

Ripoti hiyo imesema kuna uwezekano mashambulizi hayo yaliwaua mamia ya wahamiaji katika miaka ya hivi karibuni.

Kwenye ripoti hiyo, shirika hilo la kutetea haki za binadamu limenakili ushahidi kutoka kwa mashuhuda wa mashambulizi yaliyofanywa na vikosi na kuonyesha makaburi ya waliouawa katika njia zilizotumiwa na wahamiaji. Mashuhuda wamesema idadi ya vifo inaweza kufikia maelfu.

Tayari Umoja wa Mataifa umeihoji Saudi Arabia kuhusu tuhuma za vikosi vyake kuwafyatulia makombora wahamiaji, katika mtindo unaoongezeka wa mashambulizi kwenye mpaka wake wa kusini unaokaribiana na Yemen, taifa linalozongwa na machafuko.

Mgogoro wa wahamiaji na ukosefu ajira Saudi Arabia

Inakadiriwa kuwa takriban waethiopia 750,000 wanaishi nchini Saudi Arabia, na kwamba 450,000 kati yao huenda waliingia nchini humo bila vibali. Hayo ni kulingana na takwimu za shirika la kimataifa la wahamiaji IOM za mwaka 2022.

Wahamiaji na kisa cha kuuliwa Khashoggi Magazetini

Machafuko yaliyodumu kwa miaka miwili katika jimbo la Tigray lililoko kaskazini mwa Ethiopia, yalisababisha makumi ya maelfu ya watu kuyakimbia makwao.

Wahamiaji wa Ethiopia wakiwasili Addis Ababa kutoka Saudi Arabia. (Picha ya maktaba 01.04.2022)
Wahamiaji wa Ethiopia wakiwasili Addis Ababa kutoka Saudi Arabia. (Picha ya maktaba 01.04.2022)Picha: Solomon Muche/DW

Mapigano yaripotiwa nchini Ethiopia licha ya wito wa amani

Saudi Arabia, taifa linalokabiliwa na uhaba wa ajira kwa vijana, limekuwa likijaribu kuwarudisha maelfu ya wahamiaji nchini mwao Ethiopia kwa ushirikiano na Addis Ababa.

Uchunguzi kwenye video na picha wasemaje?

Shirika la Human Rights Watch lilisema lilizungumza na wahamiaji 38 wa Ethiopia, jamaa wanne wa wahamiaji waliojaribu kuingia Saudi Arabia kati ya Machi 2022 na Juni 2023, na walisema walinzi wa Saudi Arabia walifyatua risasi au vilipuzi dhidi ya makundi ya wahamiaji.

Ripoti hiyo imeeleza pia kuwa shirika hilo lilichunguza zaidi ya video 350 na picha zilizopigwa kati ya Mei 12, 2021 na Julai 18, 2023, ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii au walizopata kutoka vyanzo vingine. Walichunguza pia mamia ya picha za kilomita mraba za satelaiti zilizopigwa kati ya Februari 2022 na Julai 2023.

"Zilionesha wahamiaji waliouawa au waliojeruhiwa, kwenye kambi na katika vituo vya matibabu, jinsi makaburi yalizidi kuongezeka karibu na kambi za wahamiaji, na kwenye majia yanayotumika sasa na wahamiaji wanaojaribu kuvuka mipaka,” ripoti hiyo imesema.

Usafirishaji haramu wa binaadamu watishia watoto wa Afrika

Saudi Arabia yakana tuhuma dhidi yake

Waasi wa Kihouthi wa Yemen ambao hupata maelfu ya dola kila wiki kutokana na usafirishaji wahamiaji kinyume cha sheria kupitia mpaka huo, hawakutoa kauli walipoulizwa kufanya hivyo.

Afisa mmoja wa serikali ya Saudia ambaye alizungumza kwa sharti la kutotambulishwa, amesema ripoti hiyo ya Human Rights Watch haina msingi na haijajikita kwenye misingi ya kuaminika. Lakini hakutoa ushahidi wa kuthibitisha kauli yake.

Barua ya Saudi Arabia kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa iliyoko Geneva mnamo mwezi Machi ilisema inakana moja kwa moja tuhuma dhidi yake ya mauaji yoyote ya kimfumo kwenye mpaka wake. Ilisema pia kuwa Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa kidogo, kwa hivyo hawawezi kuthibitisha madai hayo.

Chanzo: APE