1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Homa mbaya ya mafua ya kandanda imefika hadi Berlin!"

Maja Dreyer14 Machi 2006

Ikiwa ni siku 87 tu zilizobaki hadi mashindano ya kandanda ya kombe la dunia yaanze nchini Ujerumani, mchezo wa mpira ndio unaingia uwanja wa siasa. Mkutano baina ya kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na wakuu kadhaa wamatayarisho ya kombe la dunia unawavutia pia wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHWg

Kesho usiku, Kansela Angela Merkel, atakutana na mtayarishaji mkuu wa kombe la dunia la kandanda hapa Ujerumani, Franz Beckenbauer ambaye pia ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani. Bado sio wazi ikiwa Jürgen Klinsmann, kocha wa sasa, atahudhuria mkutano huu ambao unasemekana kutohusu tu hali ya matayarisho bali pia mzozo kati ya Klinsmann na Beckenbauer. Pamoja na timu ya Ujerumani kushindwa vibaya nchini Italia, Klinsmann anakosolewa kwa sababu ya kukaa sana Marekani badala ya Ujerumani.

“Siku 87 kabla ya kombe la dunia, hakuna eneo lolote nchini hapa ambalo halihusiki na kandanda.” Haya anaandika mhariri wa gazeti la “Nordwest-Zeitung” la mjini Oldenburg. Na anaendelea kusema: “Sasa mpira unachezwa katika ikulu, mkuu wetu ayatatue matatizo yetu. Mkutano huo ambao ulipangwa zamani tayari unaonekana kama unagonga vichwa vya habari. Lakini Merkel atakuwa na busara ikiwa hatoingilia mambo ya kandanda. Lakini atawaonyesha wanaume hawa jambo muhimu: Ukitaka kuwakaribisha wageni lazima kuacha kuangalia tu maslahi ya kibinafsi na uwivu.” - ni maoni ya “Nord-West-Zeitung”.

Suala hilo linashughulikiwa pia na gazeti la “Mannheimer Morgen”. Limeandika:

“Ni mbaya mno kwamba Ujerumani baada ya timu yake kushindwa inavunjika moyo kabisa na hivyo kuharibu furaha yoyote ya kukaribia michuano ya kombe la dunia. Sasa hata kiongozi wa serikali anazingatia masuala ya soka badala ya kuyatatua matatizo ya umma, kama vile watu milioni 5 wasio na ajira au mfumo wa huduma za umma kuvunjika. Kuna jibu moja tu kwa hali hiyo: Homa mbaya ya mafua ya kandanda imefika hadi Berlin!”

Na homa nyingine imeingia katika uchumi, yaani homa ya mameneja kuziunganisha kampuni. Haya ni maoni ya wahariri baada ya kampuni ya madawa ya Merck ya Ujerumani kutangaza mpango wake wa kuinunua na kuungana na kampuni nyingine ya madawa ya Berlin, Schering, hivyo kuwa ni kampuni kubwa zaidi ya madawa nchini humo.

Gazeti la “Abendzeitung” kutoka Munich linausifu mpango huo:
“Kwa utafiti wa madawa hiyo ni habari nzuri. Mpaka sasa kampuni za madawa za Ujerumani zilikuwa ndogo mno. Kampuni kubwa kama hiyo inayopangwa inaweza kushindana na makampuni ya kimataifa. Na ni makampuni makubwa tu ambayo yana uwezo wa kifedha kutengeza dawa mpya.”

Na mwisho gazeti la “Frankfurter Rundschau” ambalo linatuhumu mpango huo ni dalili ya ugonjwa mpya. Limeandika:
“Inaonekana kuna homa ya mameneja. Yule ambaye anaugua anajisikia kama inambidi anunue kitu, bila ya kujali bei. Dalili nyingine ya homa hiyo ni kuwa na ndoto ya kuwa na madaraka makubwa. Hakuna hatari kwa mgonjwa mwenyewe. Wale watakaoathirika ni wafanyakazi, wateja na wenye hisa.”