1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hertha yamsimamisha kazi Salomon Kalou

Josephat Charo
5 Mei 2020

Hertha Berlin imemsimamisha mshambuliaji wake Salomon Kalou baada ya kutuma video kwa mtandao wa Facebook iliyomuonesha yeye na wachezaji wenzake wakisalimiana kwa mikono na kuvunja masharti ya kudhibiti COVID-19.

https://p.dw.com/p/3bnuc
Fussball Salomon Kalou
Picha: picture-alliance/SvenSimon/F. Hoermann

Klabu ya Hertha Berlin imesema Jumanne (05.05.2020) katika taarifa kwamba "hii ni tabia ya mchezaji mmoja" na kukanusha madai kwamba kikosi kizima hakizingatii utaratibu wa kutokaribiana na sheria za usafi kwa uzito unaotakiwa.

Mchezaji huyo wa Ivory Coast ameomba radhi kwa tabia yake ambayo kitengo cha ligi kinachopanga ratiba ya mechi za Bundesliga, DFL, kiliileza kwenye mtandao wa Twitter kuwa "isiyokubalika kabisa" na ambayo baadhi ya vyombo vya habari vimependekeza huenda ikavuruga matumaini ya Bundesliga kurejea tena viwanjani baada ya kusitishwa kutokana na kuzuka janga la virusi vya corona.

Hertha, ambayo imesema video hiyo ilitayarishwa baada ya kikosi kizima kutopatikana na maambukizo ya virusi vya corona, ilikiri kwamba katika sehemu moja video hiyo inawaonesha wachezaji wakisalimiana kwa mikono huku Kalou pia akionekana akitatiza upimaji wa kitabibu wa wachezaji wenzake.

"Video ya Salomon Kalou kutoka chumba cha kubadilishia nguo ilikiuka sheria msingi za timu na kuonesha tabia isiyofaa kwa hali iliyopo na haiendani na sheria za maadili za klabu," ilisema taarifa.

"Hertha BSC kwa hiyo imeamua kumsimamisha mara moja kutoka mazoezi na kucheza."

Taarifa iliongeza: "Salomon Kalou alishawishiwa na matokoe ya vipimo kuwasalimia wachezaji wenzake katika chumba cha kubadilishia nguo, wakati mwingine kwa kuwasalimia kwa mkono, kinyume na matangazo ya wazi ya afisa wa usafi."

Meneja wa Hertha, Michael Preetz, amesema Kalou ameisababishia klabu hiyo "uharibifu mkubwa wa sifa yake" na "kutoa taswira kwamba wachezaji hawalichukulii suala la corona kwa uzito."

Preetz alisema klabu hiyo ilielezea kinagaubaga suala la usafi na sheria ya kutojongeleana kwa wafanyakazi wake wote.

Kalou, mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Chelsea, Lille na Feyenoord ambaye ameichezea Ivory Coast mechi 90, ameodha radhi.

"Sikufikiria kwa kweli na nilifurahi kwamba majibu ya vipimo vyetu hayakuonesha tumeambukizwa," alisema, akiongeza kuwa ana wasiwasi mkubwa sana kuhusu hali ya janga la corona barani Afrika.

"Ningependa pia kuomba msamaha kwa wale walioonekana kwenye video ambao hawakujua nilikuwa nikionyesha video mubasahra na ambao sikutaka kuwaweka katika hali kama ile."