1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatua ya Uturuki kuingilia kijeshi Libya yaleta wasiwasi

Sylvia Mwehozi
3 Januari 2020

Umoja wa Ulaya umeelezea wasiwasi mkubwa hii leo juu ya uamuzi wa Uturuki wa kuingilia kijeshi katika vita nchini  Libya, na kuungana na Marekani, Urusi na Misri ambazo nazo zimegusia wasiwasi kama huo. 

https://p.dw.com/p/3Vgn5
Libyen Tripoli | Streitkräfte Libyens
Picha: picture-alliance/Xinhua/H. Turkia

Siku ya bunge la Uturuki lilipiga kura kuidhinisha mamlaka ya mwaka mmoja ya kuwatuma wanajeshi wake katika taifa la Afrika Kaskazini la Libya. Uturuki inajaribu kuisaidia serikali ya mjini Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya waziri mkuu Fayez al-Serraj. Serikali hiyo inakabiliwa na mashambulizi ya utawala hasimu unaongozwa na kamanda aliye na nguvu Khalifa Haftar anayepambana kuudhibiti mji mkuu Tripoli.

"Hakuna suluhisho la kijeshi kwenye mzozo wa Libya. Hatua za kuwasaidia wanaopigana katika mgogoro huo zitaidhoofisha nchi na ukanda wote", imesema taarifa ya Umoja wa Ulaya. Taarifa hiyo imesisitiza kwamba washirika wote wa kimataifa lazima waheshimu kikamilifu marufuku ya silaha iliyowekwa na Umoja wa Mataifa nchini Libya, na kuunga mkono juhudi za mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Ghassan Salame.

Türkei Istanbul | Libyens Premierminister al-Sarraj trifft Erdogan
Waziri mkuu wa serikali ya mjini Tripoli Fayez Serraj na rais Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AP Photo/Turkish Presidency

Rais Recep Tayyip Erdogan alisema serikali ya Umoja wa kitaifa GNA ya Libya iliiomba Ankara kutuma vikosi vyake. Rais wa Marekani Donald Trump alimueleza Erdogan kwamba "uingiliaji wa kigeni utafanya hali kuwa ngumu Libya", kulingana na taarifa ya Ikulu ya Marekani, White House.

Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya kigeni katika bunge la Urusi, Leonid Sluzki ameuita uamuzi wa Uturuki kuwa wenye kutia shaka. Misri ambayo ni mpinzani wa Libya kikanda, nayo ililaani kura hiyo inayodai kwamba inakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Nchi nyingine ambazo zimelaani uamuzi huo wa Uturuki ni Ugiriki, Israel na Cyprus. Kwenye taarifa ya pamoja waliyoitoa Alhamis jioni, nchi hizo zimesema kwamba, "uamuzi huo unakiuka vikali maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kudhoofisha juhudi za jumuiya za kimataifa za kutafuta suluhisho la kisiasa kwa njia ya amani katika mzozo wa Libya.

Nchi hizo zimeitolea wito Uturuki kujizuia kuyatuma majeshi yake Libya hatua ambayo itakiuka uhuru wa taifa hilo. Mnamo mwezi Novemba Uturuki na serikali ya Umoja wa kitaifa ya Libya zilisaini makubaliano yaliyo na utata juu ya ushirikiano wa kijeshi na usalama katika mipaka yake ya majini.