1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magavana kadhaa wa upinzani nchini Kenya waondolewa walinzi

18 Julai 2023

Magavana husika wameshikilia kuwa hatua hiyo haitalegeza msimamo wao kuunga mkono maandamano ya siku tatu mfululizo ya upinzani ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha, yaliyopangwa kuanza hapo keshi Jumatano.

https://p.dw.com/p/4U4jt
Kenia Präsident William Ruto
Picha: TONY KARUMBA/AFP

Hatua ya kuwaondolea ulinzi vinara wa muungano wa upinzani nchini Kenya wa Azimio, wabunge na magavana wa eneo la Nyanza imeibua shutma dhidi ya serikali kuu. Katika hatua hiyo, serikali ya kitaifa iliyo na mamlaka ya kuratibu ulinzi wa viongozi wa kisiasa kupitia wizara ya ulinzi wa kitaifa siku ya Jumatatu ilitangaza kuwaondoa walinzi hao mara moja kipindi hiki upinzani umetangaza maandamano ya siku tatu mfululizo.

Usimamizi wa idara ya polisi haujatoa maelezo kuhusu hatua hiyo

Mshauri mkuu wa maswala ya mawasiliano wa gavana wa jimbo la Kisumu Prof. Peter Anyang Nyong'o John Oywa katika mahojiano na DW ameeleza kushtushwa na uamuzi wa kumuondolea ulinzi gavana huyo na wenzake. Kulingana na Oywa, serikali ya jimbo la Kisumu imetamaushwa na hatua hiyo ikizingatiwa kuwa, ni haki ya maafisa husika kupewa ulinzi na licha ya kutaka maelezo zaidi, usimamizi wa idara ya polisi nchini haujatoa maelezo ya kwa nini wamechukua hatua hiyo.

Orengo asema hatanyamazishwa na vitisho vya serikali kuu

Waandamanaji nchini Kenya wakabiliana na maafisa wa polisi katika maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha nchini humo mnamo Julai 7 2023
Waandamanaji jijini NairobiPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Kwa upande wake, gavana wa jimbo la Siaya, James Orengo ambaye ni mmoja kati ya magavana walioathirika ameendelea kutangaza msimamo wake wa kuunga mkono maandamano ya upinzani akisema hatanyamazishwa na vitisho kutoka serikali kuu. Orengo ameeleza kuwa, ni laazima serikali ya Kenya Kwanza isikilize na kuheshimu malalamiko ya Wakenya. Kando na wawili hawa, magavana wengine ni Gladys Wanga wa Homabay na Ochilo Ayako wa Migori.

Viongozi wa upinzani wahimizwa kudumisha ushirikiano

Mwakilishi wa vijana chama cha UDA kinachounda muungano wa Kenya Kwanza jimbo la Kisumu Steven Oduor Onyiko akitoa kauli yake kuhusiana na hatua ya serikali na msimao wa maandamano wa upinzani amehimiza viongozi wa upinzani nchini kudumisha ushirikiano bora na serikali akisisitiza kuwa, ni kinaya kwa muungano huo kuipinga serikali na pia kuitegemea serikali kuwapa ulinzi. Anapendekeza upinzani kutumia nafasi yao kupitia kwa wabunge kwenye bunge la kitaifa kuwasilisha malalamiko yao badala ya kuendesha maandamano.

Viongozi mbali mbali wa Azimio wapokonywa ulinzi

Vinara wa Azimio, Raila Odinga mwenzake Kalonzo Musyoka pamoja na zaidi ya wabunge 50 wa upinzani wamepokonywa walinzi wao uongozi wa muungano huo ukidai kuwa, hatua hiyo ina nia fiche. Odinga kupitia ukurasa wake wa kijamii Twitter ameandika nikinukuu, "Kunzia jumatano, kuwa tayari kwa maandamano ya mabadiliko, Tumechoka.net'