1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimaye DRC kumzika rasmi Lumumba miaka 50 baada ya kuuawa

11 Septemba 2020

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inasema itaandaa mazishi rasmi ya shujaa wa uhuru, Patrice Lumumba, baada ya Mahakama ya Ubelgiji kusema jino la Lumumba lililoko Ubejiji linapaswa kurudishwa kwao.

https://p.dw.com/p/3iLZp
Kongo Leopoldville | Verhaftung | Patrice Lumumba
Picha: picture-alliance/dpa

Serikali ya Kongo iliupongeza uamuzi wa Mahakama ya Ubeljiji uliotolewa siku ya Alkhamis (Septemba 10), ambapo Waziri wa Haki za Binadamu wa Kongo, André Lite, alisema kwamba baada ya kurejeshwa kwa mabaki hayo, Lumumba angelifanyiwa mazishi ya kitaifa.

"Katika siku za hivi karibuni, serikali itachukuwa msimamo wa dhati. Naweza kusema kwamba kutafanyika mazishi rasmi ya kitaifa, sababu Patrice Emery Lumumba anastahili heshima hizo. Anatakiwa kuenziwa na taifa lake'', alisema waziri huyo.

Lumumba, aliyekuwa waziri mkuu wa Kongo baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru kutoka kwa Ubeljiji mwaka 1960, aliuwawa Januari 17 mwaka 1961 katika mazingira ya kutatanisha. Jino lake linadaiwa kuchukuliwa na afisa wa polisi wa Ubeljiji aliyekuwa anasaidia kuuzika mwili wake.

Baada ya miaka kadhaa ya tukio hilo, afisa huyo alielezea kwamba mwili wa Lumumba uliunguzwa kwa kutumia tindikali.

Wafuasi, familia wasubiri kwa hamu kumzika shujaa wao

Lambert Mende, msemaji wa zamani wa serikali ya Kongo na ambaye ni kiongozi wa chama kinachofuata itikadi za Lumumba, alisema kwamba kurejeshwa kwa mabaki ya Lumumba ni ishara yenye maaana kubwa kwa raia wa Kongo.

"Mabaki hayo ijapokuwa ni jino pekee, yana ishara kubwa katika kutuliza nyonyo za familia, wafuasi na raia wote wa Kongo. Sababu ikiwa mwili au sehemu ya mwili wa mtu hautarejeshwa kwa familia yake kwa ajili ya mazishi, hatuwezi kusema kwamba tulifanya msiba wa kifo cha Patrice Emery Lumumba'', alisema Mende.

Mtoto wa kwanza wa marehemu Lumumba aitwaye Francois Lumumba alisema hatua hiyo ya mahakama ya Ubeljiji ilikuwa imefungua ukarasa mpya baina ya watu wa Kongo na wa Ubeljiji.

"Ni hatua muhimu, ni ukarasa mpya uliofunguliwa. Kwa viongozi wa Kongo nitawaomba kujihusisha kikamilifu ili mabaki ya Lumumba yarejeshwe nchini mwake. Na kwa wale wa Ubelgiji ni kwamba waharakishe utaratibu huo ili mabaki hayo yarejeshwe haraka iwezekanavyo mjini Kinshasa." Alisema Bwana Francois Lumumba.

USA New York | Premierminister Kongo | 1960 Patrice Lumumba
Patrice Lumumba (katikati) wakati wa uhai wake kwenye picha hii iliyopigwa tarehe 24 Julai 1960. Picha: picture-alliance/AP Photo

Uamuzi huo wa mahakama ya Ubeljiji ulifuatia ombi la watoto wa Lulumba kwa mfalme wa Ubeljiji wa kutaka warejeshewe mabaki ya baba yao. 

Serikali ya Ubelgiji ilihusika katika kifo chake na mwaka 2002 iliomba rasmi msamaha.

Vitengo vya ujasusi vya Uingereza na Marekani pia vinadaiwa kuhusika.