1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harare. Zimbabwe yasherehekea miaka 25 tangu kupata uhuru.

18 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFLn

Rais Robert Mugabe leo ameadhimisha miaka 25 ya uhuru wa nchi yake kwa kuyaambia mataifa ya magharibi yaangalie chaguzi zao na kuacha kuiangalia Zimbabwe. Bwana Mugabe ameuambia mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Harare kuwa uchaguzi wa nchi hiyo hauhitaji kuidhinishwa na mataifa ya Ulaya na Marekani. Akaongeza kuwa uchaguzi wa Zimbabwe utaidhinishwa na Waafrika, pamoja na mataifa rafiki kutoka mataifa ya dunia ya tatu.

Bwana Mugabe amewaambia maelfu ya watu waliokusanyika katika sherehe hizo kuwa mataifa rafiki ndio yatatoa haki kwa Zimbabwe na sio Ulaya ama Marekani. Amesema kwa kuwa mataifa ya Afrika hayalazimishi kuangalia chaguzi zao kwa hiyo mataifa hayo yanapaswa kukaa mbali na masuala ya Afrika.

Chama cha Bwana Mugabe cha Zimbabwe African National Union Patriotic Front, ZANU PF kimeshinda katika uchaguzi mwezi uliopita ambao chama cha upinzani kimesema haukuwa wa haki, wakati Marekani , Uingereza na mataifa mengine ya Ulaya yameutangaza uchaguzi huo kuwa haukuwa huru na wa haki.