1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HARARE : Chama cha Mugabe chashinda uchaguzi wa bunge

2 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFRA

Chama tawala cha Rais Robert Mugabe hapo jana kimejizolea ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge ambao upinzani unadai kuwa ni wa udanganyifu mkubwa na kumshutumu kiongozi huyo mkongwe kwa kuifanya Zimbabwe kama mali yake binafsi.

Chama cha Mugabe cha ZANU-PF kimenyakuwa viti 69 vikijumuishwa na 30 ambapo wabunge wake huchaguliwa moja kwa moja na Rais kunakiweka chama hicho tawala punje moja tu kujinyakulia ushindi mkubwa wa uwezo wa kupitisha maamuzi wa theluthi mbili katika bunge lenye viti 150.

Chama cha upinzani cha Vuguvugu la Mabadiliko ya Demokrasia MDC kimejipatia viti 35 kwa kushinda katika mji mkuu wa Harare na mji wa pili kwa ukubwa wa Bulawayo wakati majimbo ya vijijini yamechukuliwa na chama cha ZANU-PF.

Mugabe mwenye umri wa miaka 81 amesema alikuwa anataka ushindi wa theluthi mbili ili kumuwezesha kufanya mabadiliko ya katiba ambayo wachunguzi wa mambo wanasema yana lengo la kumlinda kiongozi huyo asije kukumbana na usumbufu uliowakumba baadhi ya viongozi wa Kiafrika baada ya kun’gatuka.Mugabe anatazamiwa kustaafu hapo mwaka 2008.

Waziri wa zamani wa habari na aliyekuwa mshauri mkuu wa Mugabe Jonathan Moyo ameshinda katika jimbo alikozaliwa akiwa mgombea wa kujitegemea.Mugabe alitishia kukitenga kijiji cha kimaskini cha Tsholotsho kilioko kusini magharibi mwa Matebeleland iwapo wanakijiji watamkabidhi kiti hicho cha ubunge adui yake huyo mpya.

Matokeo ya uchaguzi huo wa Zimbabwe pia yameshutumiwa na Ujerumani, Umoja wa Ulaya na Marekani.