1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Hamilton Naki: Mvumbuzi wakati wa ubaguzi wa rangi

Yusra Buwayhid
28 Aprili 2020

Licha ya kukosa elimu ya juu, Hamilton Naki aliyeishi wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, alianza maisha kama msimamizi wa bustani na baadae kuja kuwa msimamizi wa maambara ya utafiti wa kisayansi.

https://p.dw.com/p/3bV9j
Projekt African Roots | Hamilton Naki - Porträt

Hamilton Naki: Mvumbuzi katika kivuli cha ubaguzi wa rangi

Hamilton Naki alizaliwa lini na wapi?

Hamilton Naki huenda alizaliwa mnamo mwaka 1926 katika kijiji cha Afrika Kusini cha Centane (kilichopo katika mkoa wa leo wa East Cape). Alizaliwa katika familia ya kimasikini, na hivyo alilazimika kuanza kujikimu kimaisha akiwa na umri mdogo. Hamilton Naki alikuwa na mke, watoto wanne wa kiume na mmoja wa kike. Alikufa kwa ugonjwa wa moyo mnamo Mei 29, 2005.

Ipi ilikuwa kazi ya kwanza ya Hamilton Naki?

Akiwa na umri wa miaka 14, baada ya kumaliza shule ya msingi, Naki alikwenda mjini Cape Town kutafuta kazi. Alipata kazi ya kutunza bustani katika Chuo Kikuu cha Cape Town. Alipewa kujumu la kutunza uwanja wa kuchezea tenisi wa chuo hicho.

Maisha ya kikazi ya Naki yalianzia wapi?

Ilipofika mwaka 1954, Naki alikuwa akifanya kazi ya kutunza wanyama katika maabara. Na ni wakati huu ambapo mtaalam wa moyo na utafiti wa sayansi Dr Robert Goetz alipogundua kuwa Naki alikuwa na ujuzi wa kipekee. Alimfundisha jinsi ya kuwaandaa wanyama kwa ajili ya upasuaji. Baadae Naki alikuja kuwa msimamizi wa maabara ya utafiti ya Taasisi ya Matibabu ya Chuo Kikuu cha Cape Town. Hivi ndivyo alivyoanza kufanya kazi na Profesa Christiaan Barnard, daktari wa moyo wa kwanza kufanya upandikizaji wa moyo wa mwanadamu.

Projekt African Roots | Hamilton Naki
Asili ya Afrika| Hamilton Naki

Je, Naki aliwahi kufanya upasuaji wa kupandikiza moyo?

Hapana, Naki hakuwahi kushiriki katika upasuaji wakupandikiza moyo. Wakati huo, Afrika Kusini ilikuwa ikiongozwa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Kama mtu mweusi, hakuruhusiwa kufanya kazi katika chumba cha upasuaji. Kwa hakika, wahudumu wa afya weusi walikuwa hawaruhusiwi kisheria kuwasogelea wagonjwa weupe. Mchango wa Naki ulikuwa katika utayarishaji wa maabara na utafiti kuhusu njia mpya za upasuaji.

Vipi Naki alichangia katika upasuaji wa kwanza wa kupandikiza moyo wa binadamu?

Naki hakuhudhuria upandikizaji huo wa kwanza wa moyo wa binadamau mnamo Desemba 3, 1967, ambapo timu ya madaktari wa upasuaji iliyoongozwa na Christiaan Barnard ilipoutoa moyo wa Denise Darvall aliyeaga dunia na kuupandikiza kwa Louis Washkansky.

Kulingana na Makumbusho ya Heart of Cape Town, iliyofunguliwa kuwaenzi wale wote waliochangia katika upandikizaji huo wa kwanza wa moyo, Naki alianza kufanya kazi na Chris Barnard kama msaidizi wake wa kuwachoma sindano ya nusukaputi wanyama kabla ya upasuaji. Kulingana na makala ya mwaka 2014 ya chuo kikuu cha upasuaji nchini Uingereza, Royal College of Surgeons, "Naki alishiriki katika juhudi za awali za kutafuta njia ya kufanya upandikizaji wa moyo. Alihusika katika kumpa nusukaputi mbwa kwa kutumia pampu, aliyekuwa akifanyiwa majaribio katika maambara ya upasuaji. Kwa mantiki hii, alikuwa sehemu ya timu iliyomsafishia njia ya mafanikio Barnard.

Projekt African Roots | Hamilton Naki
Asili ya Afrika | Hamilton Naki

Vyanzo tofauti vimekuwa vikisisitiza kuwa Hamilton Naki alishiriki katika upandikizaji wa kwanza wa moyo. Uvumi huu ulisambaa vipi?

Utawala wa ubaguzi wa rangi ulijitahidi kuficha mafanikio ya watu weusi walio wengi nchini Afrika Kusini, lakini serikali iliyotawala baada ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi nchini humo ilikuja kufichua udhalimu huo. Udhalimu alioupitia Naki kikazi, uliwakuta raia wengi weusi wa Afrika Kusini na kadri miaka ilivyosonga mbele ulikuzwa na kutiwa chumvi. Kufuatia kifo chake, Mei 29, 2005, vyombo vingi vya habari vya kuaminika vilichapisha wasifu wa Naki na kusema kwamba alishiriki katika upasuaji wa kwanza wa kupandikiza moyo wa binadamu. Baadae vyombo hivyo vya habari vililazimika kurekebisha machapisho hayo. Katika miaka ya hivi karibuni, familia yake pia imeonyesha hasira , ikidai kwamba Naki ndiye aliyeufanya upasuaji huo wa kupandikiza moyo wa binadamu. Mtoto wake Thembinkosi Naki, anasema, "Udhalimu huu ulimmchoma sana. Chris alipata tuzo zote, lakini baba yangu hakupata kitu.”

Naki: Msimamizi wa maambara, bila ya elimu ya juu.

Je, Christiaan Barnard alikuwa na mtazamo gani kuhusu mchango wa Hamilton Naki?

Katika miaka yake ya baadaye, Christiaan Barnard alikuja kuwa muwazi zaidi juu ya mchango wa Hamilton Naki na heshima aliyonayo kwake. Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press mwaka 1993 alisema, "Iwapo Hamilton angepata fursa ya kufanya upasuaji, angekuwa daktari mzuri sana.” Na mwaka 2001, miaka michache kabla ya kifo chake, aliliambia gazeti la Uingereza la Daily Telegraph kwamba Naki alikua "mmoja wa watafiti wazuri wa wakati huo kwenye uwanja wa kupandikiza mioyo ... Alikuwa na ujuzi bora wa kiufundi kuliko mimi, haswa linapokuja suala la kushona, na alikuwa na mikono mizuri sana."

Je, Naki alipata tuzo zozote?

Mwaka 2002, Rais wa zamani wa Afrika Kusini Thabo Mbeki alimpa Naki tuzo ya 'The Order of Mapungubwe' yenye heshima ya juu zaidi nchini humo, ambayo wanapewa raia wa Afrika Kuisni waliochangia katika mafanikio makubwa ya nchi hiyo.

Mwaka 2003, alipokea Shahada ya Heshima ya Sayansi ya Tiba kutoka Chuo Kikuu cha Cape Town.

Projekt African Roots | Hamilton Naki
Asili ya Afrika| Hamilton Naki

Jina la Hamilton Naki linakumbukwa vipi?

Mnamo mwaka 2007, ulianzishwa msaada wa masomo ya utabibu uliopewa jina la Hamilton Naki. Lengo la msaada huo ni kuwasaidia wanafunzi wa Afrika Kusini wanaotoka kwenye familia za kimaskini na wanaotaka kufanya utafiti wa kisayansi wa kiwango cha juu. Aidha Taasisi ya Taifa ya Utafiti nchini humo, imezindua Tuzo ya Hamilton Naki inayotolewa kwa watu waliofanikisha utafiti wa kiwango cha kimataifa katika mazingira magumu. Na mnamo mwaka 2017, uwanja wa Salazar Palin mjini cape Town, ambao uko mbele ya Hospitali ya Christiaan Barnard, ulipewa jina la Hamilton Naki.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel