1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Hamas yapendekeza mpango wa kusitishwa kwa mapigano

7 Februari 2024

Kundi la wanamgambo la Hamas limependekeza mpango wa kusitishwa kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza kwa muda wa miezi minne na nusu na hatimaye kumaliza vita kabisa katika eneo hilo

https://p.dw.com/p/4c7hk
Moshi unapaa kutoka kwa majengo mjini Rafah Kusini mwa Ukanda wa Gaza wakati wa shambulizi la Israel mnamo Januari 25, 2024 katika mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Israel na wanamgambo wa kundi la Hamas
Moshi unaotokana na shambulizi la Israel katika Ukanda wa GazaPicha: AFP/Getty Images

Kulingana na rasimu ya pendekezo hilo iliyoonekana na shirika la habari la Reuters, mpango huo wa kundi la Hamas unaangazia awamu tatu ambazo kila moja itachukua muda wa siku 45.

Yaliomo kwenye pendekezo la Hamas

Pendekezo hilo litaliwezesha kundi hilo linalotambuliwa kuwa la kigaidi na Israel na washirika wake, kubadilishana mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina, kuanzishwa kwa ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza, kujiondoa kabisa kwa vikosi vya Israel na kubadilishana miili ya watu waliouawa kwenye mapigano hayo.

Soma pia:Blinken awasili Mashariki ya kati kwa mara ya tano

Kulingana na pendekezo hilo la Hamas, wanawake wote mateka wa Israeli, wanaume walio chini ya umri wa miaka 19, wazee na wagonjwa, wataachiwa huru katika awamu ya kwanza ya siku 45 kwa kubadilishana na kuachiliwa kwa wanawake na watoto wa Kipalestina kutoka jela za Israel.

Blinken ashinikiza makubaliano ya baada ya mapigano

Haya yanajiri wakati Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Antony Blinken, ambaye yuko ziarani katika eneo hilo kwa mara ya tano tangu kuzuka kwa vita hivyo kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo la Hamas mwezi Oktoba mwaka jana, anajaribu kuendeleza mazungumzo hayo ya kusitisha mapigano, huku akishinikiza makubaliano makubwa zaidi ya baada ya mapigano, ambapo Saudi Arabia huenda ikaanzisha mahusiano ya kawaida na Israel baada ya kuweko mwelekeo wazi na wa kuaminika wa kuanzishwa kwa taifa la Kipalestina.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa kwa ushirikiano na katibu mkuu wa Jumuiya ya NATO Jens Stoltenberg mjini Washington mnamo Januari 29, 2024
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani - Antony BlinkenPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Akizungumzia pendekezo hilo la Hamas wakati wa mkutano na wanahabari nchini Qatar hapo jana, Blinken alisema kuwa bado kuna kazi nyingi za kufanya lakini wanaendelea kuamini kwamba kuna uwezekano wa makubaliano na wataendelea kufanya kazi kwa bidii kufanikisha hilo.

Saudi Arabia yasema haitarejesha mahusiano na Marekani hadi matakwa yake yatakapotimizwa

Katika hatua nyingine, Saudi Arabia imeiambia Marekani kwamba haitaanzisha uhusiano na Israel hadi taifa huru la Palestina "litakapotambuliwa'' rasmi.

Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema lazima Israel isitishe mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza na vikosi vyote vya Israeli lazima viondoke katika eneo hilo lililozingirwa.

Soma pia:Hamas yazingatia pendekezo la mapatano lililoridhiwa na Israel

Kauli hiyo ya leo imetolewa kujibu matamshi ya msemaji wa Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa nchini Marekani, John Kirby, ambaye aliwaambia waandishi wa habari hapo jana Jumanne kwamba mazungumzo ya kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Saudi Arabia naIsrael "yanaendelea" na kwamba Washington "imepokea maoni chanya" kutoka kwa pande zote mbili kwamba ziko tayari kuendelea na mazungumzo hayo.

Jeshi la Israel lasema limewauwa mamia ya wapiganaji wa Kipalestina

Ndani ya Gaza kwenyewe, jeshi la Israel limesema leo kuwa vikosi vyake vimewauwa mamia ya wapiganaji wa Kipalestina katika mji wa Khan Younis ulio kusini mwa ukanda huo ndani ya masaa 24 yaliyopita.

Katika taarifa yake, jeshi hilo pia limesema kuwa limepata idadi kubwa ya silaha na kufichua mahandaki katika eneo hilo.