1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ya wakimbizi Ulaya ni mbaya

Lillian Urio21 Juni 2005

Esteban Beltran mkurugenzi nchini Spain wa Amnesty International, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, ameonya kwamba wakimbizi na wahamiaji walio katika nchi za Umoja wa Ulaya wako hatarini.

https://p.dw.com/p/CHgL

Pia Oberoi, mtaalam wa Amnesty International juu ya masuala ya wakimbizi na waomba uhamiaji, ameliambia shirika la habari la IPS kwamba serikali zilizo katika Umaja wa Ulaya na nchi nyingine za Magharibi, zinahangaika kwa kuwapeleka wakimbizi hao katika nchi nyingine badala ya kuwasaidia.

Oberoi amesema sera hiyo haizingatii kwamba wengi wao hupelekwa katika nchi zinazo ongozwa na madikteta, ambao hawaheshimu haki za binadamu kabisa. Alisema haya mjini Madrid mwanzoni mwa wiki katika sherehe za kuhidhinisha siku ya Wakimbizi duniani.

Beltran na Oberoi waliwakilisha ripoti mpya iliyoitwa, Spain: Mpaka wa Kusini. Huku wakikumbushia vifo vilivyotokea mwezi wa Juni tarehe 13, mwaka huu, vya wanawake 6 na watoto 6, kutoka Kusini mwa Afrika. Waliozama maji baada ya boti yao duni kupinduka, karibu na mji wa bandari wa Moroko wa Tangier.

Siku tatu baadaye, watu 13 waliokolewa na polisi wa maji wa Spain. Watu hao walikuwa wanavuka bahari, kutoka Afrika kuelekea Ulaya, kwa njia isiyokuwa ya kihalali. Walikuwa kwenye boti yao siku kumi bila chakula wala maji. Watu wengine 11 walikufa wakati wa safari hiyo na waliwatupa majini.

Waliookolewa walikuwa wanaume 12 na mwanamke moja kutoka nchi za Afrika Magharibi za Ghana na Mali. Baharia wa meli inayosafirisha wanyama waliwagundua maili 120, kutoka visiwa vya Kanary. Wakavuta boti hiyo na meli yao na kuzitaarifu mamlaka husika za Spain.

Mda mfupi kabla ya matukio hayo mawili, polisi wa Spain waligundua kundi la watu 59, wanaojaribu kuingia Ulaya kinyume na sheria, wakiwemo watoto 33.

Mwaka 2004, wahamiaji 1,575 walio chini ya umri wa miaka 18 na wasio na vibali walikamatwa wakijaribu kuingia Spain.

Ripoti hiyo kutoka Amnesty International, inaonyesha hali ya wasiwasi kusini mwa Spain katika fukwe wa za bahari pamoja na visiwa vya kanary, kusini-magharibi mwa Afrika. Hali hiyo ni sababu ya wahamiaji, wanaohatarisha maisha yao, kwa kujaribu kuifikia Ulaya na kuvuka bahari kwa vyombo visivyo salama.

Ripoti hiyo pia imesema kwamba polisi wa Spain huwanyanyasa watu hao kabla ya kuwarudisha nchini mwao au kuwapeleka nchi nyingine, bila kujaribu kuhakikisha kwamba sio waomba hifadhi.

Beltran amesema mamlaka husika na vyombo vya habari nchini Spain wanachangia kuwaongezea wakimbizi matatizo, kwa kuwaita wote wahamiaji wasio halali. Hawazingatii kwamba kuna wale wanao omba hifadhi kwa sababu hawawezi kurudi nchini mwao, wakati mwingine kutokana na matatizo ya kisiasa.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu, limesema kwamba halipingi suala la serikali kusimamia uhamiaji na masuala ya wageni kuingia nchini.

Ripoti hiyo imeongeza kwamba tendo la serikali za Ulaya la kuwajibika zaidi na kusimami uhamiaji, limepunguza umuhimi wa kuwalinda wakimbizi.

Amensty pia iliweka wazi uchunguzi uliofanywa juu ya jinsi nchi za Ulaya zinavyoshughulikia suala la wakimbizi na wahamiaji.

Nchini Aaustria, kuna mwomba hifadhi aliyekataa kuondoka kambini, mwaka 2004, kwenda kusikiliza kesi yake na akanyanyaswa, pamoja na kuzimiwa sigara kwenye mabega.

Wakati nchini Ubelgiji ripoti hiyo inasema kwamba wale wanaofukuzwa nchini kwa nguvu, wana ondolewa katika mazingira mabaya yasio heshimu binadamu.

Hali nchini Ufaransa pia sio nzuri, vituo vya wakimbizi na wahamiaji vimedhoroteka na kushuka chini ya viwango vya kimataifa. Haswa kwa watoto walio kwenye vituo, wanaosubiri kurudishwa makwao, bila wazazi wala walezi.

Mashirikia yanaowasaidia wakimbizi na wahamiaji katika mipaka yamesema kwamba kuna visa vya watoto kuzuiwa kuundana na wazazi wao, ambao tayari wamo nchini.

Pia kuna matukio mbalimbali ya nchini Ugiriki. Likiwemo tukio la mwezi Desemba mwaka 2004, polisi wanashutumiwa kuwanyanyasa na kuwaumiza kundi la watu 60 waomba hifadhi kutoka Afghanistan. 17 kati yao walikuwa chini ya umri wa miaka 18.

Uchunguzi huo umeeleza kwamba polisi hao waliwapiga ngumi, mateke, wakawanyanyasa kijinsia na kuwatishia na bundiki, majumbani mwao na katika kituo cha polisi mjini Athens.