1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Hali ya sintofahamu yagubika taarifa za kifo cha Prigozhin

24 Agosti 2023

Inaaminika kuwa mkuu wa kundi binafsi la kijeshi la Urusi, Wagner, Yevgeny Prigozhin pamoja na maafisa wa ngazi ya juu wa kundi hilo, wamekufa katika ajali ya ndege iliyotokea Jumatano usiku.

https://p.dw.com/p/4VX0J
Russland Prigoschin soll bei Absturz gestorben sein | Tver
Waokozi wakiondoa miili kwenye ajali ya ndege inayosadikiwa kumbeba pia kiongozi wa Wagner, Yevgeny PrigozhinPicha: AP Photo/picture alliance

Shirika la usafiri wa anga la Urusi, Rosaviatsiya, limesema Prigozhin na maafisa sita wenye vyeo vya luteni walikuwemo ndani ya ndege binafsi iliyoanguka mara tu baada ya kupaa kutoka Moscow, ikiwa na wafanyakazi watatu. Waokoaji walifanikiwa kuipata haraka miili yote 10, na vyombo vya habari vya Urusi vimenukuu vyanzo vya kampuni ya Wagner, ambavyo vimethibitisha kifo cha Prigozhin.

Ajali hii ni ya kupangwa?

Ajali hiyo inaonekana kama mauaji ya kupangwa, miezi miwili baada ya kuongoza uasi dhidi ya vikosi vya kijeshi vya Urusi.Marekani na maafisa wengine wa mataifa ya Magharibi walikuwa wakitarajia kwa muda mrefu Rais wa Urusi Vladmir Putin kumuadhibu Prigozhin, licha ya kuahidi kumfutia mashtaka katika makubaliano ambayo yalimaliza uasi wa Juni 23 hadi 24.

Alipoulizwa na waandishi habari kuhusu mkasa huo, Rais wa Marekani Joe Biden, alisema hana taarifa za kutosha kuhusu kile kilichotokea, lakini hashangazwi. ''Lakini sishangai. Hakuna kitu kinachotokea Urusi bila ya Putin kuhusika. Sina jibu la kutosha,'' alibainisha Putin.''

Russland Prigoschin soll bei Absturz gestorben sein | Tver
Mabaki ya ndege binafsi iliyoanguka huko Tver, UrusiPicha: AP Photo/picture alliance

Wafuasi wa Prigozhin wamedai kuwa ndege hiyo ilidunguliwa kwa makusudi, ingawa madai kama hayo hayangeweza kuthibitishwa. Wapinzani wengi na wakosoaji wa Putin wameuawa au kuugua vibaya katika majaribio ya mauaji. Hakuna afisa yeyote wa serikali ya Urusi au shirika la Rosaviatsiya ambaye amethibitisha kama kweli Prigozhin amekufa.

Televisheni inayoiunga mkono Ikulu ya Urusi, Kremlin ya Tsargrad imeripoti kuwa mwili wa Prigozhin ulikuwa umetambuliwa, lakini bado wanasubiri vipimo vya sampuli za vinasaba, DNA.

Kamanda mwingine hajulikani alipo

Mauaji hayo yamefanyika siku ambayo vyombo vya habari vya Urusi viliripoti kuwa kamanda wa zamani wa ngazi ya juu ambaye iliripotiwa alikuwa na mahusiano na Prigozhin, Jenerali Sergei Surovikin amefukuzwa kazi, kama kamanda wa kikosi cha anga cha Urusi kilichoko nchini Ukraine. Surovikin hajaonekana hadharani tangu ulipofanyika uasi.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameonya dhidi ya uvumi kuhusu ajali hiyo. Akizungumza Alhamisi na kituo cha redio cha Ujerumani cha Deutschlandfunk, Baerbock amesema hakuna hitimisho la haraka ambalo linaweza kutolewa.

Russland Jewgeni Prigoschin Statement in Rostow-am-Don
Mkuu wa kundi binafsi la kijeshi la Urusi, Wagner, Yevgeny Prigozhin Picha: Press service of "Concord"/REUTERS

Akizungumzia mustakabali wa kundi la mamluki la Wagner, mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani amesema ana hofu kuwa Urusi itaendelea na mchezo wake wa kejeli, ikiwa au isipokuwa na Wagner, na sio tu nchini Ukraine, bali zaidi barani Afrika.

Ufaransa: Kuna mashaka juu ya chanzo cha ajali

Ufaransa kwa upande wake imesema kuna mashaka kuhusu chanzo cha ajali hiyo ya ndege. Msemaji wa serikali, Olivier Veran amekiambia kituo cha televisheni cha France 24, kwamba hawajui mazingira ya ajali hiyo, na wanaweza kuwa na mashaka.

Alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais Biden, kwamba mambo yanayotokea Urusi, Putin anahusika, Veran amekubali kuwa kama kanuni ya msingi, huo ni ukweli unaoweza kuthibitishwa. ''Prigozhin alimgeuka Putin, na kwamba alichokifanya hakitenganishwi na sera za Putin ambaye alimpa majukumu ya kutekeleza dhulma kama mkuu wa Wagner,'' alifafanua Veran.

(AFP, DPA, Reuters)