1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto wa wakimbizi jimboni Rutshuru wanakosa elimu

2 Agosti 2023

Wakibimbizi katika jimbo la Rutshuru huko mashariki mwa DRC wameelezea kugadhabishwa na kitendo cha watoto wao kunyimwa elimu ambapo ni takribani miaka miwili sasa hawajaenda shule.

https://p.dw.com/p/4Ugtq
DR Kongo | Nach der Flut in Kinshasa
Picha: Justin Makangara/REUTERS

Raia waliokimbia vita kati ya waasi wa M23 na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi Kongo huko wilayani Rutshuru na ambao wanaishi ndani ya kambi za wakimbizi nje kidogo na mji wa Goma, wameelezea kugadhabishwa na kitendo cha watoto wao kunyimwa elimu ambapo ni takribani miaka miwili sasa hawajaenda shule.

Wananchi hao wanaopitia hali hiyo wameitaka serikali ya Kongo kuanza kuwapatia elimu wanafunzi, licha ya waasi wa M23 kudhibiti vijiji vyao. Akiwa pamoja na watoto wake saba katika hema chakavu, Bibi Florence Nyazoga, anayeishi ndani ya kambi ya Kanyaruchinya nje kidogo na mji wa Goma, anaelezea wasiwasi wake kutokana na watoto wake kukosa kwenda masomo.

Watoto hawaendi shule kwa takribani miaka miwili.

Uganda Kisoro Flüchtlinge DR Kongo
Kina mama wakiwa katika kambi ya wakimbizi mjini Rutshuru.Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Takribani miaka miwili hivi sasa, waasi wa M23 wamevikalia baadhi ya vijiji wilayani Rutshuru ambako maelfu wa raia waliyakimbia makazi yao na hivyo kukatizwa kwa shughuli za kielimu kote katika eneo hilo linalokumbwa na ukosefu wa usalama. Bwana Mashagiro mkuu kiongozi wa mji mdogo wa Rugari, ulioko umbali wa kilometa 35 kaskazini mwa mji wa Goma na anayeishi kambini hapo, anasema ombi lake ni upatikanaji wa amani na kuanzishwa kwa shule.

Wakati huohuo, katika tangazo lao mapema mwanzoni mwa juma hili, waasi hao wa M23 wameahidi pia kuanzisha hule ifikapo mwezi wa Septemba kulingana na kalenda iliyotolewa na serikali ya Kinshasa, tangazo lililoibua hisia mseto miongoni mwa raia.

Soma zaidi:HRW: Waasi wa CODECO walifanya mauaji ya kikatili Ituri, DRC

Tangu kuzuka upya kwa vita hivi kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23, mamia ya wafanyakazi katika sekta ya elimu wilayani Rutshuru walilazimika kufungasha virago ili kukimbia machafuko na kwenda kutafuta fursa nyingine ili kujipatia riziki. Ikiwa umesalia mwezi moja kabla ya kufunguliwa kwa shule, wizara ya elimu nchini Kongo bado haijathibitisha kufunguliwa kwa shule katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa M23, jambo linalowatia hofu raia katika maeneo hayo.