1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali nchini Syria

Oumilkher Hamidou28 Agosti 2012

Jeshi la Syria limeshambulia eneo la mashariki la mji mkuu Damascus katika wakati ambapo jumuia ya kimataifa inalaani mauwaji ya Daraya, na kutoa mwito uchunguzi ufanywe" haraka na bila ya mapendeleo".

https://p.dw.com/p/15xue
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon(kushoto) na mjumbe mpya wa kimataifa kwa Syria Lakhdar BrahimiPicha: picture-alliance/dpa

Shirika la haki za binaadam la Syria lenye makao yake makuu mjini London nchini Uingereza linazungumzia kuhusu mapigano makali yaliyoanza tangu alfajiri ya leo katika mitaa ya mashariki ya mji mkuu Damascus huko Zamaika, Qaboon, Jubar na Ein Tarma, huku mkuu wa vikosi vya waasi akiliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP, lengo halisi la jeshi la Syria safari hii ni eneo la Ghuta, mashariki ya mji mkuu Damascus.

Hujuma hizi zinatokea licha ya lawama na laana za jumuiya ya kimataifa, baada ya jumla ya watu 190 kuuliwa kufuatia mashambulio ya jana kote nchini Syria.

Lawama za walimwengu zinaongozwa na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-Moon, aliyetoa mwito hapo jana uchunguzi huru ufanywe kujua nani walikuwa nyuma ya kuuliwa mamia ya raia kataika mji wa Daraya,wiki iliyopita.

Shirika la haki za binaadam la Syria limesema miili mengine saba imegunduliwa Daraya na kuifanya idadfi ya walioliwa kufikia watu 340 kufuatia kile ambacho wanaharakati wanakitaja kuwa "mashambulio makali ya siku tano,mauwaji ya kiholela na msako wa vikosi vya serikali toka nyumba moja hadi nyengine."

Daraja Syrien Massaker
Mauwaji ya kiholela ya DarayaPicha: dapd

Marekani imezitaja ripoti kuhusu mauwaji ya Daraya kuwa "ushahidi wa mwisho kwamba Assad hathamini maisha ya binaadam,Uingereza inazungumzia juu ya "ukatili wa aina mpya huku Umoja wa Ulaya ukilaani mauwaji hayo na kusema si jambo linaloweza kukubalika hata kidogo".

Wakati huo huo rais mpya wa Misri Mohammed Mursi anaeitembelea jamhuri ya umma wa China ,amezitolea mwito Urusi na China zisaidie kumng'owa madarakani Bashar Al Assad."Hakuna tena wakati wa mageuzi na majadiliano amesema,la muhimu ni kuzuwia damu isiendelee kumwagika.

Syrien - Kämpfe in Aleppo
Mapigano yameripuka huko AleppoPicha: Getty Images

Pendekezo la rais Francois Hollande wa Ufaransa kuutaka upande wa upinzani uunde serikali ya mpito haliungwi mkono na serikali ya Marekani.Serikali ya mjini Washington inashauri badala yake upande wa upinzani ushirikiane kwa dhati na "wasyria wote tangu wa ndani mpaka walioko nje"

Baadhi ya wadadisi wanahisi upande wa upinzani unadhibitiwa na wafuasi wa nadharia kali ya madhehebu ya Sunni na wanaweza kulipiza kisasi dhidi ya jamii ya wachache ya Alawi na kutishia kwa namna hiyo kuendeleza mapigano ya kikabila.

Mwandishi:Hamidou Oummilkhheir/Reuters/AFP

Mhariri:Josephat Charo