1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali bado ni tete mjini Nairobi

MjahidA23 Septemba 2013

Makabiliano makali ya risasi na mlipuko umesikika katika jengo la Westgate mjini Nairobi, ambako jeshi la Kenya linakabiliana na baadhi ya wapiganaji wa kundi la Al shabaab wanaowazuia mateka kadhaa katika jengo hilo.

https://p.dw.com/p/19mVy
Jumba la Westgate
Jumba la WestgatePicha: Reuters

Watu takriban 69 wameuwawa katika shambulizi hilo la Jumamosi katika eneo la maduka la Westigate huku watu wengine zaidi ya 100 wakipata majeraha mabaya. Kwa upande wake shirika la msalaba mwekundu limesema kwa sasa watu 63 hawajulikani waliko.

Ni takriban zaidi ya saa 48 na bado polisi wanajaribu kuwaokoa mateka ndani ya jengo hilo la Westgate.

Polisi waliokuwa katika eneo hilo walilazimika kukimbilia mahali salama wakati palipotokea mlipuko huo.

Jeshi la Kenya likikabiliana na Al Shabaab
Jeshi la Kenya likikabiliana na Al ShabaabPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Jeshi la Kenya limesema kwa sasa limedhibiti ghorofa ya kwanza katika jengo hilo na wanatarajia kufanya shambulizi la mwisho dhidi ya wanamgambo hao wa Al Shabaab ambao wanaaminika kuwateka raia kwa ajili ya kujikinga na mashambulizi kutoka kwa vikosi vya usalama.

Kulingana na mkuu wa polisi nchini Kenya, David Kimaiyo, wamefanikiwa kuwaokoa baadhi ya waliotekwa na kwa sasa wale waliobakia ndani na wanachama hao wa Al shabaab ni wachache sana.

Magaidi hao walifika katika jengo la Westgate siku ya Jumamosi na kuanza kuwamiminia risasi raia waliokuwa katika mkahawa huo ambako watu 69 waliuwawa na wengine zaidi ya 150 kupata majeraha mabaya.

Al Shabaab wazungumzia tukio

Msemaji wa kundi la Al shabaab linaloaminika kuwa na mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda, Ali Mohamud Rage ameonya kwamba wale walioshikwa mateka watalipa kufuatia hatua ya jeshi la Kenya kupeleka vikosi vyake Somalia vinavyopambana na kundi hilo la Kigaidi.

Msemaji huyo amesema iwapo Kenya inataka amani basi ni lazima iondoe jeshi lake nchini Somalia.

Hata hivyo rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameapa ya kwamba kundi hilo litakabiliwa vikali na vyombo vyake vya usalama. "Tutawaadhibu wale waliotekeleza kitendo hiki na tutawaadhibu kwa nguvu zetu zote," Alisema Rais Kenyatta wakati alipokuwa anatoa hotuba yake kwa Umma hapo jana akisema kuwa mpwa wake aliyekuwa na mchumba wake waliuwawa katika shambulizi lililotekelezwa na magaidi hao wa Al Shabaab.

Kundi la Al Shabaab
Kundi la Al ShabaabPicha: Mohamed Abdiwahab/AFP/Getty Images

Kwa sasa maafisa wa usalama nchini Kenya wanasaidiana na wenzao wa Israel pamoja na polisi kutoka Uingereza, na Marekani katika kukabiliana na wapiganaji hao. Bado miili kadhaa inaaminika kutapakaa ndani ya jengo hilo kufuatia shambulizi la siku ya jumamosi.

Ruto arudi nyumbani kutokana na shamabulizi la Jumamosi

Huku hayo yakiarifiwa hii leo Jumatatu mahakama ya uhalifu wa kivita ilioko The Hague Uholanzi ICC imemruhusu makamu wa rais nchini Kenya William Ruto kurudi nyumbani kwa muda wa wiki moja ili kuwa na wakenya katika wakati huu wa shambulizi.

Ruto na mshitakiwa mwenzake mwandishi habari Joshua Arap Sang wanakabiliwa na makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu wanayodaiwa kufanya katika ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007.

Makamu wa rais William Ruto
Makamu wa rais William RutoPicha: picture alliance / Kyodo

Wakati huo huo raia watatu wa Uingereza, wanawake wawili raia wa Ufaransa, watu wawili kutoka Canada akiwemo mwanadiplomasia mmoja, mwanamke mmoja raia wa China, wahindi wawili, raia mmoja wa Korea Kusini na mwanamke mmoja wa Uholanzi ni miongoni mwa waliouwawa katika shambulizi hilo.

Hii ni kulingana na taarifa kutoka kwa serikali ya Kenya iliotangaza kuwa mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Awoonor, aliye na umri wa miaka 78 pia aliuwawa katika shambulizi la kigaidi.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/dpa/Reuters

Mhariri: Josephat Charo