1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakainde Hichilema ashinda uchaguzi wa rais Zambia

Daniel Gakuba
16 Agosti 2021

Tume ya uchaguzi wa Zambia imemtangaza kiongozi wa upinzani, Hakainde Hichilema kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Alhamis iliyopita. Rais aliyekuwepo Edgar Lungu, ametishia kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/3z1vb
Afrika Sambia Oppositionsführer Hakainde Hichilema
Hakainde Hihilema, Rais Mteule wa ZambiaPicha: picture-alliance/Photoshot/Xinhua/Penglijun

Hata kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, wafuasi wa Hakainde Hichilema na chama chake cha United Party for National Development, UPND walijimwaga katika mitaa ya mji mkuu Lusaka na kushangilia, ilipodhihirika kuwa mgombea wao alikuwa akielekea kwenye ushindi, hii ikiwa mara yake ya sita kujitosa katika kinyang'anyiro cha urais wa Zambia.

Soma zaidi: Rais wa Zambia asema uchaguzi 'haukuwa hura na wa haki'

Alfajir ya leo, mbele ya waandishi wa habari na wadau wengine, mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi ya Zambia Esau Chilu, baada ya matokeo kutoka majimbo 155 kati ya 156, amemtangaza Hichilema kuwa mshindi.

''Hichilema, Hakainde, S; milioni mbili, mia mbili na kumi elfu, na mia saba na hamsini na saba. Kwa hiyo namtangaza Hichilema Hakainde S, kuwa rais mteule wa jamhuri ya Zambia, leo tarehe 16 Agosti mwaka 2021.'' Amesema Esau Chilu.

Awashukuru wapiga kura wake

Sambia Unruhen in Lusaka
Wafuasi wa chama cha UPND wakishangilia katika mitaa ya mji mkuu, LusakaPicha: Salim Dawood/AFP

Mara baada ya kutangazwa mshindi, Hichilema ambaye ni mfanyabiashara tajiri aliweka picha yake katika mtandao wa twitter akiwa mbele ya wafuasi wake, na kuweka ujumbe usema, ''Asante Zambia''.  Hii ilikuwa mara ya sita kwake kugombea wadhifa huo, mara tano za mwanzo akiambulia patupu.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, rais aliyekuweko madarakani Edgar Lungu wa chama cha Patriotic Front ameambulia kura 1,814,201. Lungu amekuwa mamlakani kwa miaka sita, na alijaribu kila awezelano kupata muhula mwingine, licha ya kupoteza umaarufu kutokana na kudorora kwa hali ya maisha, na kukosolewa kuukandamiza upinzani.

Soma zaidi:  Wazambia wanashiriki katika uchaguzi wa rais na Bunge

Wakati wa kampeni ya uchaguzi huu uliomalizika, wanajeshi walimzuia Hichilema kufanya kampeni katika maeneo muhimu ukiwemo mkoa wa Shaba, kwa kisingizio cha hatua za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Ahadi ya kuufufua uchumi kwa kuwavutia wawekezaji

Hichilema mwenye umri wa miaka 59 na msomi mwenye shahada ya uchumi, ameahidi kurejesha imani ya wawekezaji, lakini anairithi nchi yenye mzigo mkubwa wa madeni, mfumko wa bei na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira.

Edgar Chagwa Lungu Präsident Sambia
Edgar Lungu, rais wa Zambia ambaye ameshindwa uchaguziPicha: UNTV/AP/picture alliance

Hapo jana, Kambi ya Rais Edgar Lungu ililalamika ikisema uchaguzi huu haukuwa wa haki, ikidai kwamba mawakala wao walishambuliwa na kufukuzwa kutoka baadhi ya vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo, waangalizi wa kimataifa wamesifu mchakato wa uchaguzi huo, wakisema ulikuwa wazi na wenye mipangilio mizuri. Wamesifu pia uitikiaji wa wapigakura, uliokuwa katika kiwango cha asilimia 70.9.

Soma zaidi: Zambia yatangaza siku 21 kuomboleza kifo cha Kaunda

Katika uchaguzi mkuu uliopita kinyang'anyiro pia kilikuwa baina yaEdgar Lungu na Hakainde Hichilema, wakati huo Lungu alipita kwa kumzidi Hichilema kwa kura 100,000 tu.

 

afpe, rtre