1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Haiti: Kashfa ya ngono kwenye soka yaibua mazito

5 Juni 2020

Mkuu wa shirikisho la kandanda nchini Haiti, Yves Jean-Bart anaendelea kukanusha kutenda makosa yoyote licha ya madai ya unyasasaji wa kingono yanayomkabili.

https://p.dw.com/p/3dJUM
Haiti | Yves Jean Bart, Präsident des haitianischen Fußballverbandes | Sexuelle Gewalt
Picha: Getty Images/A. Schneider

Mkuu wa shirikisho la kandanda nchini Haiti, Yves Jean-Bart amekuwa na mamlaka makubwa kwa miongo  kadhaa na licha ya madai ya unyanyasaji wa kingono na kukiri kwamba amezaa na mcheza mpira wa hapo  zamani, na licha ya kufanyiwa uchunguzi, Jean-Bart bado anaendelea kukanusha kutenda makosa yoyote.     

Wanasoka wanawake na makocha wananyamazishwa juu ya madai ya unyanyasi wa kiongono kwenye shirikisho la soka la nchini Haiti na pia juu ya madai yanayoelekezwa kwa Jean-Bart , rais wa muda mrefu wa shirikisho hilo. Kocha mmoja wa Haiti aliyekabaliana ana kwa ana na njama zao alitoa ushahidi kwa DW kuhusu Jean-Bart.

Hata hivyo, alibadilisha ushahidi wake baada ya kutakiwa atoe maelezo zaidi. Badala yake kocha huyo alisema hakuna wanasoka wanawake anaowafundisha waliotendewa uhalifu wa kingono.

Mwanaharakati maarufu wa haki za wanawake, Pascale Solages ameeleza kuwa watu wanaotendewa uhalifu huo huamua kunyamaza kimya kutokana na kuona aibu na hasa ikiwa madai hayo yanamkabili mtu mkubwa.

Mwanaharakati huyo amesema Jean-Bart ni mtu mwenye mamlaka makubwa na kwa hivyo anaweza kuwatisha wale wanaotendewa uhalifu, familia zao na hata taasisi. Solages ameeleza kwamba ikiwa anayehusika na uhalifu ni mtu mwenye usemi mkubwa, fisadi na mwenye fedha nyingi, inakuwa vigumu zaidi kwa mwanamke kupata haki.

Haiti | Yves Jean Bart, Präsident des haitianischen Fußballverbandes | Sexuelle Gewalt
Rais wa shirikisho la soka la Haiti Yves Jean-Bart anatuhumiwa kuwanyanyasa kingono wachezaji wa kike na kuwatishia kuwauawa iwapo watasema chochote.Picha: picture-alliance/AP Images/D. N. Chery

DW imezungumza na watu kadhaa ili kuthibitisha madai hayo ambayo kwa mara ya kwanza yalifichuliwa na gazeti la Uingereza la ''The Guardian'' mwishoni mwa mwezi uliopita.

Klabu moja nje ya Haiti imesema inatoa msaada kwa mchezaji kandanda mmoja wa zamani. Klabu hiyo imesema ina wasiwasi mkubwa na maafisa wake wameeleza kuwa madai yaliyotolewa yanawasumbua roho kwa kiwango kikubwa.

Madai ya wahanga kutishiwa kifo na familia zao

Gazeti la The Guardian linadai kwamba Jean-Bart aliwalazimisha wanasoka wanawake kwenye kituo cha mafunzo cha taifa kujihusisha naye kingono. Gazeti hilo la Uingereza pia limedai kwamba wachezaji wapatao wawili walilazimika kutoa ujauzito.

Kwa mujibu wa gazeti hilo wanawake waliotendewa uhalifu wa kingono pamoja na familia zao walitishiwa kuuawa kwa sababu ya kufichua unyanyasaji waliofanyiwa.

Mpaka sasa Jean-Bart bado hajajibu maombi ya DW ya kujibu maswali yetu. Hata hivyo polisi nchini  Haiti inasonga mbele na uchunguzi. Jean-Bart amekanusha vikali madai yanayotolewa juu yake na amesema kuwa madai hayo ni njama za kutaka kumng'oa kwenye shirikiso la kandanda ambalo linamuunga mkono.

Wakati huo huo, Shirikisho la mchezo wa kandanda duniani, FIFA limemsimamisha kazi Jean -Bart kwa muda wa miezi mitatu ili kuruhusu uchunguzi ufanyike wakati kamati ya maadili ikiliagilia shauri hilo. FIFA pia imeunda kamati maalumu itakayokusanya ushahidi wa ugani. Wakati Jean-Bart  amesimamishwa, nafasi yake inashikiliwa na naibu wake.

Haiti | Yves Jean Bart, Präsident des haitianischen Fußballverbandes | Sexuelle Gewalt
Jean-Bart amesimamishwa na nafasi yake inashikiliwa na naibu wake.Picha: Imago/J. Abelard

Jean-Bart ameongoza kandanda kwa muda wa miaka 20 nchini Haiti. Kwa mujibu wa taarifa za watu kadhaa, kiongozi huyo amejenga mamlaka makubwa, ndani na nje ya Haiti katika medani ya soka, na kwamba ana mahusiano na wanasiasa na vyombo vya habari. Jean-Bart kwa sasa ni mkurugenzi wa kituo kimoja cha radio ya mambo ya biashara. 

Njia mojawapo anayotumia ili kujijengea ushawishi ni kuwapa watu visa za kusafiria ambazo ni vigumu kupatikana Haiti ambayo ni miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani. Kwa njia hiyo anawapa zawadi waandishi habari na wanamichezo.    

Mpaka sasa hakuna ushahidi juu ya madai yanayotolewa dhidi ya Jean-Bart. Mtaalamu wa hali za migogoro wa chama cha soka cha Haiti, FHF Evan Nierman ameiambia DW kwamba madai yanayotolewa hayana msingi.

Ameeleza kuwa chama hicho cha soka kinaunga mkono kufanyika uchunguzi wa kina kwa sababu ameeleza kwamba chama hicho kinataka kuthibitisha kuwa hakuna mambo kama hayo ndani ya taasisi hiyo. Hata hivyo, chama hicho cha kandanda kinapinga kuweka mambo wazi.


Polisi inaendelea na uchunguzi, lakini mpaka sasa Jean-Bart bado hajafunguliwa mashtaka ya kutenda uhalifu. Mwanasheria mkuu wa jimbo amemuhoji Jean-Bart na ameeleza kuwa haiwezekeni kumfungulia mtu mashtaka ya uhalifu bila ya ushahidi.

Chanzo: DW