1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Habari za ulimwengu kutoka DW mjini Bonn

oummilkheir31 Januari 2005
https://p.dw.com/p/CEH4

Walimwengu wanasifu moyo wa wairaq walioteremka kupiga kura licha ya vitisho vya makundi ya kigaidi.

Viongozi wa umoja wa Afrika wameamua kurefusha wadhifa wa mwenyekiti wa sasa wa umoja huo rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria

Na wahamiaji wa kiyahudi wanaandamana kupinga mpango wa waziri mkuu wa kuwahamisha toka Gaza hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Baghdad:

Waziri mkuu wa Iraq,Iyad Allawi amewasifu na kuwashukuru wanajeshi wa nchi shirika na wananchi wa Iraq kwa jinsi uchaguzi mkuu ulivyopita nchini humo.Katika mkutano na waandishi habari,waziri mkuu Iyad Allawi amesema uchaguzi huo ni ushindi dhidi ya magaidi.Licha ya vitisho vya mashambulio ya kigaidi,idadi kubwa ya wairaq wameteremka vituoni ,kuliko vile ilivyotarajiwa ,kulichagua bunge na mabaraza ya majimbo.Kamisheni kuu ya uchaguzi inakadiria asili mia 60 ya waliojiandikisha wametoa sauti zao.Idadi kubwa zaidi imeripotiwa katika maeneo ya kusini wanakoishi watu wa madhehebu ya shiya na katika maeneo ya kaskazini wanakoishi wakurd.Katika maeneo wanakoishi watu wa madhehebu ya sunni vituo vingi vya kupiga kura vilikua vitupu.Mashambulio kadhaa yameripotiwa katika maeneo mbali mbali na kugharimu maisha ya watu zaidi ya 30.Waziri mkuu Iyad Allawi amesema raia wa kigeni wamekamatwa kuhusika na mashambulio hayo..Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi yanatazamiwa kutangazwa siku sita kutoka sasa na matokeo rasmi,kati kati ya wiki ijayo.Bunge jipya la mpito la Iraq litakua na jukumu la kutunga katiba na kufungua njia ya kuitishwa uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu.

New-York:

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan amewatolea mwito wairaq wasuluhu.Katibu mkuu Kofi Annan amesema muhimu kuliko yote ni kwa pande zote nchini Iraq kushirikiana na kutunga katiba mpya ya nchi yao.Rais George W. Bush wa Marekani ameutaja uchaguzi wa jana nchini Iraq kuwa ni "ufanisi".Amesema mjini Washington " wananchi wa Iraq wamejitambulisha na mfumo wa kidemokrasi."Serikali ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani mjini Berlin imeutaja uchaguzi wa Iraq "kua hatua muhimu kuelekea mfumo wa kidemokrasi."Waziri mkuu wa Uengereza Tony Blair amesema uchaguzi wa Irak ni pigo la mauti kwa magaidi wa kimataifa.Ufaransa imeutaja uchaguzi huo kua ni ushindi wa wananchi wa Iraq na hatua muhimu kuelekea demokrasia.Katika nchi za Ghuba,maoni ya magazeti yanatofautiana kati ya furaha na hadhari kuhusiana na uchaguzi wa Iraq.

Berlin.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Joschka Fischer ameutaja uchaguzi wa Iraq kua hatua muhimu kuelekea demokrasia.Amesema wairaq wanastahiki kusifiwa kwa kutokubali kutishika na kuudhihirishia ulimwengu wamepania kuwajibika na kuiongoza nchi yao katika njia ya amani na demokrasia.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Joschka Fischer amesema kilichosalia kwa sasa ni kutiwa njiani azimio nambari 1546 la umoja wa mataifa kuhusu utaratibu wa kisiasa nchini Iraq.Bwana Joschka Fischer ameongeza kusema Ujerumani iko tayari pamoja na washirika wake kusaidia utaratibu huo chini ya usimamizi wa umoja wa mataifa.

London:

Wanajeshi 15 wa kiengereza wameuwawa ndege yao ilipodondoka nchini Iraq.Habari hizo zimetangazwa na duru za kijeshi toka London.Waziri mkuu Tony Blair amethibitisha pia habari hizo,lakini bila ya kutaja idadi ya waliouwawa.Chanzo cha kuanguka ndege hiyo ya kijeshi hakijulikani.Ilikua njiani kuelekea mji wa kati wa Balad.

Abuja:

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Kofi Annan,akihutubia mbele ya viongozi wa Umoja wa Afrika mjini Abuja,ametetea haja ya kuimarishwa mafungamano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa mataifa,ili,kama alivyosema "kuyafikia malengo ya millenium hadi ifikapo mwaka 2015."Wakati huo huo duru za kidiplomasia mjini Abuja zinasema mikutano ijayo ya kilele ya Umoja wa Afrika itafanyika nchini Libya,mwezi July ujao na Sudan, January mwakani.Mikutano yote miwili itaongozwa na mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika,rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria.Duru hizo zimeongeza kusema wadhifa wa rais Obasanjo kama mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika umerefushwa hadi january mwakani.Viongozi wa Afrika wamepitisha uamuzi huo katika mkutano wao wa nne wa kilele katika mji mkuu wa Nigeria-Abuja jana jioni.Mkutano huo wa kilele umelengwa kuzungumzia mizozo ya bara la Afrika,hasa nchini Ivory Coast,jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo,Sudan na Somalia na haja ya kutumwa vikosi vya kulinda amani katika maeneo hayo.

Jerusalem:

Washauri wakuu wa waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon wamepangiwa kukutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleeza Rice baadae hii leo mjini Washington.Vyombo vya habari vya Israel vimesema washauri wa masuala ya kisiasa Dov Weisglass na Shalom TURDJEMAN na mwambata wa kijeshi jenerali Yoav Galant watakutana leo usiku na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,Condoleeza Rice,mazungumzo yatakayohudhuriwa pia na balozi wa Israel mjini Washington Dany Ayalon.Kwa mujibu wa radio Israel,mazungumzo hayo yatahusiana na ziara ijayo ya mwanadiplomasia huyo wa kimarekani nchini Israel na Palastina february sita na sabaa ijayo.Washauri wa waziri mkuu Ariel Sharon watamkabidhi pia waziri Condoleeza Rive ripoti kuhusiana na mawasiliano ya ahivi karibuni kati ya Israel na Palastina na fursa iliyojitokeza ya kuwekwa chini silaha.Wakati huo huo wahamiaji zaidi ya laki moja wameandamana mjini Jerusalem dhidi ya mpango wa waziri mkuu Ariel Sharon wa kuwaondowa wanajeshi na wahamiaji wa kiyahudi toka Gaza hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu.

Nairobi:

Watu sita,wakiwemo wakenya wanne na wataliana wawili wanatazamiwa kuhukumiwa hii leo baada ya kugunduliwa madawa ya kulevya mwezi uliopita mijini Mombasa na Malindi.Madawa hayo ya kulevya yanayopindukia tani moja yanasemekana yametokea Colombo na kulengwa kuingizwa katika masoko ya ulaya kupitia Uholanzi.Watuhumiwa wote sita wamedai hawahusiki na biashara ya madawa ya kulevya.Rais mwengine wa Kenya,George Kiragu anakabiliwa na mashtaka kama hayo nchini Uholanzi,na mwengine Railton Muthungu anasakwa kwa tuhuma kama hizo.Bangi hiyo inatajikana kua nyingi kabisa,kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru mwaka 1963.Kiongozi wa shughuli za forodha na madhamana wengine kadhaa walikamatwa na kuhojiwa kabla ya akuachiwa huru baadae.Viongozi wa Kenya wanahofia nchi hiyo ya Afrika mashariki isije ikageuzwa kivukio cha biashara ya kimataifa ya madawa ya kulevya kuelekea Ulaya.