1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoBrazil

Gwiji wa soka Pele aaga dunia akiwa na umri wa miaka 82

30 Desemba 2022

Pele, lejendari wa timu ya taifa ya Brazil aliyekulia kwenye umaskini na hatimaye kuwa mmoja wa wanamichezo wakubwa duniani, amefariki jana Alhamisi akiwa na umri wa miaka 82.

https://p.dw.com/p/4LYu7
Fussballspieler Pele
Picha: Eamonn M. McCormack/Getty Images

Hospitali ya Albert Einstein iliyoko mjini Sao Paulo, ambako Pele alikuwa akipokea matibabu, imesema gwiji huyo wa kandanda alifariki saa tisa na dakika 27 alasiri, kutokana na viungo vyake kushindwa kufanya kazi.

Pele amekuwa akiugua saratani ya utumbo.

Kifo cha Pele, ambaye ni mtu pekee aliyeshinda Kombe la Dunia la FIFA mara tatu kama mchezaji mwaka 1958, 1962 na mwaka 1970, kilithibitishwa kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram.

"Msukumo na upendo ndio sifa zilizopamba safari ya Mfalme Pele, aliyefariki dunia leo," ndio ujumbe ulioandikwa kwenye akaunti yake ya Instagram na kuongeza "aliiletea dunia furaha kutokana na kipaji chake katika soka, alizuia vita, alifanya kazi za kijamii duniani kote na kueneza kile alichoamini kuwa tiba ya matatizo yetu yote: upendo."

Risala za rambi rambi zinaendelea kumiminika kutoka kile pembe ya dunia- kuanzia fani ya michezo, siasa, burudani, sanaa na tamaduni, kwa mtu maarufu aliyeiweka Brazil katika ramani ya soka duniani.

Serikali ya Rais Jair Bolsonaro, anayeondoka madarakani mnamo siku ya Jumapili, imetangaza siku tatu za maombolezo, na kusema katika taarifa kuwa Pele alikuwa mzalendo halisi, akiliinua jina la Brazil kila mahali alipokwenda.

Mrithi wa Bolsonaro, Rais mteule Luiz Inacio Lula da Silva, ameandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa, "Wabrazil wachache sana wamefanikiwa kulibeba jina la nchi yetu kama alivyofanya Pele."

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema urithi wa Pele katika soka utaishi milele. "Mchezo. Mfalme. Milele," Macron aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter.

Pele alikuwa akifanyiwa tiba ya kemikali tangu alipoondolewa uvimbe kwenye utumbo wake mnamo Septemba mwaka 2021.

Pia alikuwa na ugumu wa kutembea bila ya msaada tangu alipofanyiwa upasuaji wa nyonga mwaka 2012.

Mnamo Februari mwaka 2020, siku chache kabla ya janga la virusi vya Corona, mwanawe wa kiume Edinho alisema hali ya afya ya babake ilimfanya atumbukie katika mfadhaiko wa akili.

Fußball WM 1970 | Brasilien ist Weltmeister
Wachezaji wa Brazil wakisherehekea ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Italia katika mechi ya fainali ya mwaka 1970Picha: dpa/picture alliance

Siku ya Jumatatu, kutafanyika hafla maalum kwa ajili yake katika uwanja wa klabu ya mpira ya Santos, klabu ya nyumbani alikokulia na ambapo alianza kucheza soka lake akiwa kijana na baadaye nyota yake kung'aaa na kujipatia umaarufu mkubwa.

Baada ya hapo, gwaride lililobeza jeneza lake litapita katika mitaa ya Santos, na kupita nyumbani anamoishi mama yake mwenye umri wa miaka 100, na msafara huo kukamilika katika makaburi ya Ecumenical Memorial Necropolis, ambapo atazikwa katika hafla ya faragha.

Pele ambaye jina lake kamili ni Edson Arantes do Nascimento, alijiunga na klabu ya Santos mwaka 1956 na kuigeuza klabu hiyo ya eneo la pwani kuwa mojawapo ya majina maarufu katika soka.

Mbali na mataji ya kikanda na kitaifa, Pele alishinda Makombe mawili ya Copa Libertadores, ligi ya Amerika Kusini ambayo ni sawa na ligi ya mabingwa barani Ulaya, na Makombe mawili ya Intercontinental, mashindano ya kila mwaka yanayozikutanisha timu bora za Ulaya na Amerika Kusini.

Pele ndio mchezaji pekee kushinda Kombe la Dunia mara tatu

Pele 70. Geburtstag Flash-Galerie
Picha: AP

Alishinda Kombe la Dunia la FIFA mara tatu, mara ya kwanza akilibeba Kombe hilo la dhahabu akiwa na umri wa miaka 17 nchini Uswidi mwaka 1958, la pili akilibeba nchini Chile miaka minne baadaye, japo alikosa mechi nyingi katika michuano hiyo kutokana na majeraha, na Kombe la tatu akalishinda nchini Mexico mwaka 1970, alipowaongoza vijana wa Samba kuishushia kichapo Italia cha mabao 4-1 katika mechi ya fainali.

Timu ya taifa ya Brazil ya mwaka 1970 inachukuliwa kama kikosi bora kuwahi kutokea katika soka la kimataifa.

Pele alistaafu kuichezea Santos mwaka 1974 japo mwaka mmoja baadaye, alirudi tena uwanjani kwa mshangao wa wengi kwa kutia saini mkataba wenye donge nono na kujiunga na klabu ya New York Cosmos iliyokuwa inashiriki ligi ya Amerika Kaskazini wakati huo.

Katika maisha yake ya soka ya takriban miaka 21, alifunga kati ya mabao 1,281 na 1,283 kulingana na jinsi mechi zinavyohesabiwa.

Ulimwengu wa soka huenda usipate bahati nyengine ya kushuhudia kipaji kama alichokuwa nacho Pele, ambaye amefariki dunia kama mmoja wa malejendari katika mchezo huo unaopendwa zaidi duniani.