1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GENEVA. Iran yashinikizwa kuacha mpango wake wa nuklia.

25 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFAE

Mawaziri wa kigeni kutoka Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wanakutana na mpatanishi wa Iran mjini Geneva, Uswissi, kujadili mpango wa nuklia wa Iran. Mawaziri hao wanafanya juhudi za mwisho kuutanzua mzozo huo wa mpango wa nuklia wa Iran.

Rais wa Iran, Mohamed Khatami, amesema mazungumzo yaliyofanyika mjini Brussels hapo awali hayakuridhisha, lakini hata hivyo akasisitiza bado yako matumaini ya kuyafikia makubaliano.

Kumekuwa na hali ya wasiwasi kufuatia hatua ya Iran kutangaza kwamba imeanzisha tena shughuli zake za kuyarutubisha madini ya uranium baada ya kuzisitisha mwezi Novemba mwaka jana. Umoja wa Ulaya umeonya utaifikisha Iran mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa iwapo itaendeleza urutubishaji wa madini hayo.

Wakati huo huo, wanamgambo wa kundi la kiislamu la Basij wamefanya maandamano nje ya ubalozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani mjini Tehran, wakitaka Iran iwe na haki ya kumiliki mpango wa nuklia.

Waziri mkuu wa Luxemboug, Jean Asselborn, ameitolea wito jumuiya ya kimataifa kuizuia Iran kutengeneza silaha za kinuklia.