1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GAZA CITY : Hali ni ya wasi wasi huko Palestina

15 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCj4

Vikosi vya usalama vya kundi la Fatah lililo tiifu kwa Rais Mahmoud Abbas wa Palestina wameyafyatulia risasi maandamano ya Hamas katika Ukingo wa Magharibi na mapigano ya risasi yalizuka kati ya makundi hayo hasimu huko Gaza na ambayo yawaweka Wapalestina kwenye ukingo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kiongozi mwandamizi wa Hamas Khalil al Hayya amemshambulia vikali Rais Abbas kwa kumuuliza anaazisha vita gani kwamba kwanza alianzisha vita dhidi ya Mungu na sasa anaanzisha vita dhidi ya Hamas.Hayya alikuwa akiuhutubia umma wa wafuasi wa Hamas 100,000 waliokuwa wakifyetuwa risasi hewani na kupiga mayowe ya Mungu Mkubwa.

Waziri Mkuu wa Palestina Ismael Haniyeh akiuhutubia umma huo maneno yake yameonekana kuwa ya usuluhishi zaidi ambapo ametowa wito wa kuwepo umoja wa kitaifa lakini hakutowa wito wa kuwepo utulivu kama alivyokuwa akifanya huko nyuma wakati kunapozuka mifarakano kati ya makundi hayo mawili.

Takriban wafuasi 32 wa Hamas katika mji wa Ukingo wa Magharibi wa Ramallah walijeruhiwa kutokana na mashambulizi ya risasi ya vikosi vya Abbas baadhi yao wakiwa katika hali mbaya sana.

Machafuko hayo mapya yamekuja baada Hamas ambayo inaidhibiti serikali ya Palestina kumshutumu kiongozi mkuu wa Fatah na walinzi wa rais Abbas kujaribu kumuuwa Waziri Mkuu Ismail Haniyeh nje ya kivuko cha mpaka wa Rafah na Misri hapo jana.