1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

G7: Ukraine yatawala siku ya mwisho ya mkutano wa kilele

22 Mei 2023

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alipata fursa muhimu katika siku ya mwisho ya mkutano wa kielele wa madola saba Tajiri Zaidi ulimwenguni – G7 nchini Japan. Viongozi pia walitangaza kuzikabili Urusi na China

https://p.dw.com/p/4Rdvy
G7 Summit in Hiroshima
Picha: Susan Walsh/REUTERS

Ijapokuwa Ukraine sio mmoja wa mataifa wanachama wa G7, macho yote yalikuwa kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa siku tatu ulioandaliwa katika mji Japan wa Hiroshima.

Soma pia:Urusi na China zakosoa tamko la mwisho la mkutano wa G7

Katika hotuba yake akiwa Bustani ya Kumbukumbu ya Hiroshima, Zelensky alisisitiza jinsi ilivyo muhimu kwa ulimwengu kuwasikia watu wa Ukraine wakitoa wito wa umoja kutoka Hiroshima, mji ambao ulijengwa upya baada ya bomu la atomiki la Marekani mwaka wa 1945. "Sasa Hiroshima ni mji uliojengwa upya, na tuna ndoto ya kuijenga miji yetu ambayo sasa ni magofu na kila kijiji ambacho hakuna nyumba hata moja iliyobaki baada ya mashambulizi ya Urusi. Tuna ndoto ya kuyakomboa maeneo yetu, kama tu tulivyoyakomboa maeneo ya kaskazini ambayo yalikuwa yamekaliwa na Urusi."

G7 Gipfel in Japan, Hiroshima |  Fumio Kishida und Wolodymyr Selenskyj im Memorial Peace Park
Waziri Mkuu wa Japan Kishida alisema mkutano wa G7 ulithibitisha kuwa hakuna mshindi wa vita vya nyukliaPicha: Naoya Azuma/The Yomiuri Shimbun/AP/picture alliance

Miito ya Zelensky ya msaada katika mkutano huo, aliohudhuria tangu Jumamosi, imepata miitikio, huku Rais wa Marekani Joe Biden akifichua msaada wa ziada wa kijeshi kwa Ukraine wa dola milioni 375. Viongozi wengine wa G7 waliahidi kuendelea kutoa msaada kwa nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita. "Putin hatoivunja dhamira yetu kama alivyodhani atafanya. Miaka miwili iliyopita, karibu miaka mitatu iliyopita. tutaendelea kutoa msaada wa kiuchumi, kiutu na kiusalama kwa Ukraine ili iweze kusimama imara kwa muda inaouhitaji msaada huo."

Hakuna mshindi katika vita vya nyuklia

Akizungumza katika hafla ya kuufunga mkutano huo, Waziri wa Japan Fumio Kishida alisema ni muhimu sana kuwa G7 wameonyesha mshikamano kwa kumualika Zelensky. Kishida alizungumzia umuhimu wa kiishara wa kuandaliwa mkutano huo mjini Hiroshima. Alisema kundi la G7 limethibitisha tena kuwa hakuna mshindi katika vita vya nyuklia na vita vya nyuklia kamwe visiwahi kutokea. Mojawapo ya matukio yaliyokuwa yamesubiriwa sana katika mkutano wa G7 ni mazungumzo ya kwanza ya ana kwa ana kati ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Zelensky tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari mwaka jana. Katika mkutano wake na Zelensky, Modi aliahidi kuwa India itafanya kila liwezekanalo kusaidia kusitisha vita hivyo. India katika siku za nyuma ilisita kulaani uvamizi huo wa Urusi, na mahusiano yake ya kiuchumi na Urusi yamekosolewa kimataifa.

Themenpaket G7 Summit Hiroshima Japan
G7 ilisisitiza kutojitenga na China kiuchumiPicha: KYODO via REUTERS

Kukabiliana na China

Wakati mada ya Ukraine imeugubika mkutano wa kilele wa Hiroshima, viongozi wa G7 pia waliungana katika masuala mapana yanayohusu China, kuanzia ongezeko la shughuli za kijeshi za Beijing hadi kwa matumizi yake ya shurutisho la kiuchumi kote ulimwenguni ili kutimiza malengo yake ya kisiasa.

Ili kusisitiza lengo lao la kuondoa hatari na wala sio kujitenga na China kiuchumi, mataifa wanachama wa G7 pia yalisisitiza kuwa sera zao za kiuchumi hazijaundwa kwa ajili ya kuzuia maendeleo ya kiuchumi ya China.

Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China iliijibu tamko hilo la G7, ikisema mtizamo wa kundi hilo hauna uhalali wa kimataifa na kulituhumu kwa kile ilichosema kuwa ni kuzuia amani ya ulimwengu.

LINK: https://www.dw.com/a-65690763