1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA inalengwa kisheria katika Ligi za Ulaya

23 Julai 2024

Ligi kuu za soka barani Ulaya, zitaanzisha hatua za kisheria dhidi ya shirikisho la soka duniani FIFA kutokana na kile walichokiita “matumizi mabaya ya mamlaka” yake katika soka.

https://p.dw.com/p/4idif
 FIFA
Nembo ya shirikisho la soka duniani FIFA Picha: Philipp Schmidli/Getty Images

Muungano wa ligi za Ulaya, unaowakilisha ligi kuu 39 na vilabu 1,130 katika mataifa 33, umesema unawasilisha malalamiko yao kwa tume ya ulaya ili kulinda ustawi wa wachezaji. Malalamiko yao yanatokea kufuatia shinikizo linaloongezeka kutoka kwa ligi na vyama vya wachezaji, kuhusu idadi kubwa ya mechi na athari ya kiafya kwa wachezaji.

Ufaransa kufungua kesi dhidi ya Shirikisho la Kandanda la Argentina kufuatia ubaguzi

Taarifa ya muungano wa kimataifa wa wachezaji Fifpro imeeleza kuwa mechi za kimataifa zimekuwa nyingi kupita maelezo, na pia zinavuruga ratiba ya mechi za ligi pamoja na kuathiri afya za wachezaji. Imeongeza kuwa, shirikisho la FIFA limeweka mbele maslahi ya kibiashara, imepuuza jukumu lake kama bodi simamizi ya kandanda, na kuathiri maslahi ya kiuchumi ya ligi na ustawi wa wachezaji.

Kwa upande wake, FIFA imejitetea kwa kusema kalenda ya soka ya mwaka huu iliidhinishwa kwa kauli moja na baraza la FIFA kufuatia mashauriano ya kina yaliyohusisha pia muungano wa kimataifa wa wachezaji Fifpro na wasimamizi wa ligi kuu barani Ulaya.