FC Kolon na Hamburg zachungulia daraja la pili
5 Machi 2018Kwa upande wa Ligi ya Ujerumani Bundesliga , mabingwa watetezi na watarajiwa Bayern Munich walishinda jana kwa mabao 4-0 dhidi ya Freiburg na Bayern inayofukuzia ubingwa wa sita mfululizo , imefungua mwanya wa pointi 20 dhidi ya timu iliyoko nafasi ya pili Schalke 04 ikiwa imesalia michezo 9 ligi kumalizika. wiki hii hata hivyo timu zilizonufaika katika mchezo wa 25 ni pamoja na Schalke 04 , iliyoishinda Hertha Berlin kwa bao 1-0 na kuchupa hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi.
Borussia Dortmund iliambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya RB Leipzig na kuenguliwa kutoka nafasi ya pili hadi ya tatu, wakati RB Leipzig ilibakia katika nafasi ya 6.
Heka heka hata hivyo ilikuw katika nafasi ya kuwnia kujinasua kutoka mkiani kwa timu mbili kongwe, Hamburg SV na FC Kolon ambazo kabla ya kuingia katika mchezo wa 25 zilikuwa zinafungana kwa poinzi , zote zikiwa na pointi 17. Hamburg SV iliikaribisha Mainz 05 katika pambano la timu zinazowania kujinasua kutoka mkiani ambapo pambano hilo lilimalizika kwa sare ya bila kufungana. Matokeo hayo hayakuisaidia sana Hamburg ambayo imefikisha sasa pointi 18.
Mkurugenzi wa sporti wa Hamburg SV Jens Todt baada ya mchezo huo alikuwa na haya ya kusema.
"Ni jambo la kusikitisha kwamba hatukuweza kushinda mchezo ule. Licha ya mbinyo mkali na kuudhibiti mchezo, kwa muda wa dakika 30 na licha ya nafasi kadhaa tulizopata. Nafasi zilikuwapo, za kushinda. Tulipaswa kushinda, na uwezekano ulikuwapo kama nilivyosema. Hatukuweza tu kufunga bao, na mfanyaiko ni mkubwa."
FC Kolon
Mshambuliaji raia wa Peru Claudio Pizarro amekuwa mchezaji wa nne mwenye umri mkubwa kufunga bao katika Bundesliga wakati FC Kolon ilipopata bao la kuongoza nyumbani dhidi ya VFB Stuttgart kabla ya mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Mario Gomez kujibu kwa kufunga mabao 2 na kuipa ushindi timu yake wa mabao 3-2 ugenini.
Pizarro mwenye umri wa miaka 39, aliipatia bao FC Kolon iliyoko mkiani kabisa kwa msimamo wa ligi bao katika dakika ya saba na sasa amepachika wavuni takriban bao moja katika kila mchezo wa Bundesliga katika muda wa miaka 20. Lakini data hizo hazikuisaidia klabu hiyo kupata matumaini ya kubakia katika ligi daraja la kwanza kwani bado imesalia kuwa timu ya mwisho miongoni mwa timu 18 za Bundesliga. Huyu hapa kocha wa timu hiyo Stefan Ruthenbeck.
"Katika muda wa dakika 44 tlicheza kandanda safi kabisa, tulipaswa kuongoza kwa mabao 2-0 ama 3-0. Kwa makosa ya mchezaji , ambayo hayapaswi kutokea tena , tuliteleza na kuwa nyuma. Tulizinduka tena mwanzoni mwa kipindi cha pili na kisha tukarudi tena nyuma. Nafikiri pia tungetumia nafasi tulizopata tungekuwa mbele bila shaka, kutokana na nafasi za wazi tulizozipata. Kwa hiyo inaumiza, lakini hakuna sababu ya kulalmika tu. Tunapaswa kuangalia mbele na tuone , iwapo dhidi ya Bremen tunaweza kupata kitu."
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe
Mhariri: Yusuf Saumu