1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fayulu ayapinga matokeo ya uchaguzi mahakamani

12 Januari 2019

Mshindi wa pili katika uchaguzi wa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Martin Fayulu amewasilisha pingamizi katika Mahakama ya Katiba kuyakataa matokeo ya uchaguzi akisema kuwa yaligubikwa na udanganyifu.

https://p.dw.com/p/3BSPv
DR Kongo nach Wahlen Martin Fayulu Anhänger
Picha: Reuters/B. Ratner

Fayulu amesema kuwa matokeo ya uchaguzi wa Desemba 30 yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi, CENI yalikuwa yamepangwa na ametoa wito wa kuhesabiwa upya kwa kura hizo. Mahakama ya Katiba ina siku saba ya kuisikiliza rufaa hiyo.

Fayulu anayapinga matokeo ya uchaguzi wa Desemba 30 yaliyompa ushindi Felix Tshisekedi, pia kutoka upande wa upinzani na amesema kuwa Tshisekedi ameshinda uchaguzi huo kutokana na mpango wa siri uliofikiwa kati yake na Rais anayeondoka madarakani, Joseph Kabila.

Muungano wa vyama vya upinzani unaoongozwa na Fayulu na unaojulikana kama Lamuka unadai kuwa kiongozi wao ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 61, hiyo ikiwa ni kulingana na waangalizi 40,000 wa uchaguzi kutoka Kanisa Katoliki. CENI, imesema kuwa Fayulu amepata asilimia 34 ya kura zilizohesabiwa, huku Tshisekedi akishinda baada ya kupata asilimia 38.

DR Kongo Politiker Felix Tshisekedi
Rais mteule wa DRC, Felix TshisekediPicha: Getty Images/AFP/T. Charlier

Fayulu amewaambia waandishi habari kwamba miongoni mwa mambo anayotaka ni pamoja na kubandikwa kwa karatasi za matokeo nje ya vituo vya kupigia kura. Aidha, Toussaint Ekombe, ambaye ni wakili wa Fayulu amesema kiongozi huyo anataka kufutwa kwa matokeo ya awali yaliyotangazwa na CENI, na kumpa Tshisekedi ushindi. Akizungumza leo na waandishi habari nje ya mahakama hiyo, Ekombe amesema rufaa hiyo iliwasilishwa jana Ijumaa.

CENI imevunja sheria ya uchaguzi

Fayulu amesema anaamini kuwa Mwenyekiti wa Ceni, Corneille Nangaa amekiuka sheria ya uchaguzi wa Desemba 30, katika kumchagua mrithi wa Rais Kabila. Hata hivyo, Nangaa amesema kuna njia mbili tu za kuzichukua hivi sasa: moja ni kuyakubali matokeo rasmi ya uchaguzi, au kufutwa kwa uchaguzi huo na kuendelea kumuweka madarakani Rais Kabila hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.

''Wananiita mimi ni askari wa watu na sitowaangusha watu wangu,'' alisema Fayulu. Amebainisha kuwa pingamizi aliloliwasilisha mahakamani linajumuisha ushahidi kutoka kwa mashahidi waliokuwepo kwenye vituo vya kupigia kura nchini Kongo.

Ulinzi mkali katika makaazi ya Fayulu

Wakati huo huo, vikosi vya usalama nchini Kongo vimeyazingira makaazi ya Fayulu pamoja na kwenye mahakama alikokuwa akitarajiwa kwenda kuwasilisha pingamizi la kuyakataa matokeo ya uchaguzi huo. Watu walioshuhudia wamesema kuwa wanajeshi na polisi waliyazingira maeneo hayo, kabla Fayulu hajawasilisha pingamizi lake mahakamani.

Kongo Wahl Polizei Symbolbild ARCHIV
Askari wakipiga doria mjini KinshasaPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Wafuasi kadhaa wa Fayulu waliokusanyika nje ya hoteli yake iliyopo mjini Kinshasa pamoja na makaazi yake, walikuwa wakiimba nyimbo za kumpinga Rais Kabila pamoja na rais mteule Tshisekedi, huku wakihisi kwamba kuzingirwa kwa maeneo hayo ni jaribio la kumtisha Fayulu.

Hayo yanajiri wakati ambapo muungano wa vyama vinavyoiunda serikali ya Kongo inayoondoka madarakani umepata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika pamoja na ule wa urais. Matokeo hayo yametangazwa  leo alfajiri na CENI.

Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA, Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba