1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA yaunda mfumo wa kuripoti ukiukwaji wa haki za binadamu

Bakari Ubena Kalika Mehta
4 Julai 2024

Katika michuano ya Euro 2024 inayoendelea nchini Ujerumani, shirikisho la soka barani Ulaya UEFA liliunda jukwaa la mtandaoni la kuwasilisha malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/4hrfN
Nembo ya michuano ya Euro 2024 nchini Ujerumani
Nembo ya michuano ya Euro 2024 nchini UjerumaniPicha: Michael Memmler/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Athari na alama za kudumu kufuatia michuano hii ya Euro 2024 vinaweza kushuhudiwa mbali na uwanja wa mpira. Mashindano ya mwaka huu tayari yameshuhudia kuibuka kwa wachezaji wengi chipukizi pamoja na matokeo ya kushangaza kama ushindi wa Georgia dhidi Ureno na kadhalika.

Lakini uamuzi wa Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA kupitisha tamko linalohusu haki za binadamu kabla tu ya kuanza kwa mashindano haya, unaweza kuwa na manufaa zaidi kwa wachezaji, mashabiki na hata hata wafanyakazi wanaojihusisha na masuala ya soka.

Fomu ya mtandaoni iliundwa ili kuripoti masuala yoyote yanayohusu haki za binadamu, lakini pia kutoa jibu stahiki na azimio la papo hapo kutoka kwa jopo la mawakili walioajiriwa na UEFA ili kushughulikia malalamiko hayo.

Euro 2024 | Mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Nicolas Füllkrug
Euro 2024 | Mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Nicolas FüllkrugPicha: Marc Schueler/IMAGO

Awali, hakukuwa na mfumo rasmi wa kuwasikiliza mashabiki, waandishi wa habari na wafanyakazi waliokabiliana na tatizo fulani, kwani hakukuwa na taarifa zilizo wazi kuhusu taasisi inayoshughulikia matatizo hayo.

Kwa hivyo, mashabiki waliathiriwa na matatizo wakati wa matukio ya UEFA kama vile fainali ya Euro mwaka 2021 huko Wembley na fainali ya Ligi ya Mabingwa ya mwaka 2022 huko mjini Paris. Wakati huoz, watu hawakufahamu mahali wala jinsi ya kuwasilisha malalamiko yao kutokana na vitendo vya dhuluma na ukandamizaji dhidi yao.

Andrea Florence, mkurugenzi wa shirika la Sport & Rights Alliance, aliangazia umuhimu wa UEFA kujumuisha wadau mbalimbali wa soka kama vilabu, ligi, mashirikisho ya kitaifa, vyama vya wachezaji na taasisi za Ulaya ili kuunda utaratibu mzuri wa malalamiko.

Sauti za mashabiki kupewa kipaumbele 

Mashabiki wa soka wakati wa mechi ya Euro-2024 kati ya Uturuki na Austria
Mashabiki wa soka wakati wa mechi ya Euro-2024 kati ya Uturuki na AustriaPicha: Georg Hochmuth/APA/picturedesk.com/picture alliance

Ronan Evain, mkurugenzi mtendaji wa mashabiki wa Soka barani Ulaya, anasema jambo la muhimu zaidi ni kujumuishwa kwa mashabiki katika kipindi cha mashauriano, jambo lililomaanisha kuwa sasa watakuwa na utulivu zaidi wa kiakili wanapokuja kuhudhuria dimba kuliko hapo awali.

Katika viwanja 10 kunakochezwa mechi hizo za Euro 2024 na maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya mashabiki maarufu kama "Fan Zone", kuna mabango yanayowaelekeza watu kuhusu jinsi ya kuripoti malalamiko yao.

Soma pia: EURO 2024: Germany yatinga robo fainali lakini hali bado ni tete

Zaidi ya hayo, kumeanzishwa katika kila uwanja eneo linaloitwa "chumba salama" ambalo ni mahsusi kwa ajili ya watu wanaohisi kukabiliwa na kitisho cha moja kwa moja au hata vitendo vya ubaguzi.

Bwana Evain amesema haki za binaadamu ni muhimu kote ulimwenguni na kila mtu anapaswa kujisikia salama akiwa uwanjani bila kujali asili, jinsia wala uwezo wake. Na kwamba mfumo huo ni njia ya kuhakikisha kuwa kila mtu anaweza kujisikia salama kadri iwezekanavyo na mahali popote alipo.

Wanasheria wa kujitegemea kupokea malalamiko

Sanamu inayoashiria Haki na Sheria huko Roemerberg, Frankfurt am Main, Ujerumani.
Sanamu inayoashiria Haki na Sheria huko Roemerberg, Frankfurt am Main, Ujerumani.Picha: Ute Grabowsky/photothek/picture alliance

Ili kuhakikisha uhuru wa mchakato wa kuripoti malalamiko hayo na kuhakikisha utatuzi wa haraka, UEFA iliajiri kampuni ya wanasheria ya Ujerumani ya Rettenmaier kushughulikia malalamiko yoyote yanayoletwa kupitia mtandaoni. Kujumuishwa kwa kampuni ya mawakili kumesaidia kuhakikisha uwezo wa kuwasilisha malalamiko bila kujulikana na pia uwezekano wa kufikiwa kwa maazimio ya haraka.

Soma pia: EURO 2024: Turkey na Netherlands zatinga robo fainali

Licha ya mchakato huo kucheleweshwa kidogo na kuwa na dosari kadhaa, wadau wa soka wanaamini kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya usawa, amani, utulivu na haki kwa wale wote wanakutana viwanjani kuanzia wachezaji, wakufunzi, mashabiki na wafanyakazi mbalimbali. Wadau hao wameongeza kuwa hii ni hatua kubwa ya maendeleo na bila shaka itatoa mwongozo kwa mashindano yajayo.

(DW)