1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yazindua mfumo wa malipo kwa Iran kuepuka vikwazo

1 Februari 2019

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimezindua mfumo wa kibiashara kuzisaidia kampuni za Ulaya zinazofanya biashara halali na Iran kuepuka vikwazo vya Marekani.

https://p.dw.com/p/3CYdJ
Gymnich-Treffen Rumänien Frankreich und Deutschland in Bukarest
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas (kulia), waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian (kushoto) na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Jeremy Hunt (katikati) wakitoa tamko wakati wa mkutano wa mawaziri wa Umoja wa Ulaya mjini Bucharest, Romania, Januari 31, 2019.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Alexandru

Umoja wa Ulaya unatumai kuwa mfumo huo maalumu wa malipo uliosubiriwa kwa muda mrefu utasaidi kuyanusuru makubaliano ya nyuklia kwa kuiruhusu Iran kuendelea kufanya bishara na kampuni za Ulaya licha ya Marekani kurejesha vikwazo baada ya Rais Donald Trump kujiondoa ghafla kwenye makubaliano hayo mwaka uliopita.

Mataifa hayo matatu ya Ulaya yaliyosani mkataba wa mwaka 2015 uliodhibiti shughuli za nyuklia za Iran na kuilegezea vikwazo vikali vya kiuchumi, yamezindua mfumo huo ambao umekuwa katika maandalizi kwa miezi kadhaa, wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje mjini Bucharest. 

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif alikaribisha habari hiyo, na kusema wanaendelea kuwa tayari kushiriki mazungumzo yenye kujenga na Ulaya kwa misingi ya usawa na kuheshimiana.

Lakini maafisa wa Marekani wamepinga wazo kwamba mfumo huo mpya utakuwa na athari zozote kwenye juhudi za kuiwekea shinikizo la kiuchumi Iran, na kutoa onyo jipya kwa yeyote anayefikiria kufanya biashara na taifa hilo.

Wakati taasisi hiyo mpya iliyopewa jina la Instex, ni mradi wa serikali tatu, itaidhinishwa rasmi na wanachama wote 28 wa Umoja wa Ulaya.

Bucharest Gymnich EU Aussenminister
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakikutana mjini Bucharest, Romania, Januari 31, 2019.Picha: Ministry of Foreign Affairs Romania

Marekani yauonya Umoja wa Ulaya

Kampuni hiyo ilisajiliwa mjini Paris siku ya Jumanne ikiwa na mtaji wa euro 3,000 pamoja na bodi ya usimamizi yenye wajumbe kutoka Ufaransa, na Ujerumani na inaongozwa na Muingireza.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa - Jeremy Hunt, Heiko Maas na Jean-Yves Le Drian, wamesema katika taarifa ya pamoja kwamba Instex itasaidia kufanikisha biashara halali kati ya Ulaya na Iran, ikijikita mwanzoni kwenye sekta muhimu zaidi kwa raia wa Iran -- kama vile famasia, huduma za afya and bidhaa za kilimo cha chakula.

Instex bado haijaanza kufanya kazi na inahitajika pia Iran iundwe mfumo sambamba wa kwake, kulingana na duru kutoka serikali ya Ufaransa -- jambo ambalo linaweza kuchukua muda kukamilisha.

Wakati inalenga kampuni ndogo na za wastani, chanzo hicho cha serikali ya Ufaransa kilisema itatuma ujumbe muhimu kwa Iran kuhusu dhamira ya Ulaya kuendeleza mkataba wa Nyuklia.

Marekani imeuonya Umoja wa Ulaya dhidi ya kujaribu kukwepa vikwazo vyake dhidi ya Iran, huku mataifa ya Ulaya pamoja na mengine yaliyosaini makubaliano hayo Urusi na China, yakisema Iran haijakiuka wajibu wake wa makubaliano hayo na inapaswa kuachwa ifanye biashara.

Shirika la atomik la Umoja wa Mataifa limehakiki utekelezaji wa Iran kuhusu wajibu wake mara 13 na hata mkurugenzi wa shirika uchunguzi la Marekani CIA, alisema wiki hii kuwa Tehran ilikuwa inaheshimu mkataba huo, hatua iliyomkarisha rais Trump.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae,afpe,afptv

Mhariri: Josephat Charo