1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU: Yarejesha vikwazo kwa Urusi kwa kuichokoza Ukraine

17 Desemba 2021

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamevirejesha vikwazo walivyoiwekea Urusi mwaka 2014 baada ya kuinyakuwa rasi ya Crimea huku wakiihimiza Urusi kurejea katika meza ya mazungumzo ikiionya itawajibishwa iwapo itaivamia Ukraine.

https://p.dw.com/p/44QGD
Russland Militärübungen
Picha: Sergey Pivovarov/Sputnik/picture alliance

Wakizungumza wakati wa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya, viongozi hao wamekubaliana kuvirejesha vikwazo vya kiuchumi kwa Urusi kutokana na hatua yake ya kuinyakuwa rasi ya Crimea inayoaminika kumilikiwa na Ukraine.

Viongozi hao pia walikubaliana kwamba vikwazo vyovyote vipya vinapaswa kuwajumuisha maafisa wa kijeshi wa Urusi  wanaohusika kupanga uwezekano wa kuivamia Ukraine kijeshi  pamoja na rais wa Urusi na familia zao. Pia huenda ikajumuisha kufungiwa kwa fedha  na kufikia  huduma fulani katika Umoja wa Ulaya pamoja na marufuku ya kusafiri na Urusi kuondolewa katika mfumo wa malipo ya kimataifa.

soma zaidi: Umoja wa Ulaya wasisitiza ushirikiano na Ulaya Mashariki

Viongozi hao wanachana wa mataifa 27 yanayounda Umoja wa Ulaya pia wameihimiza Urusi kuondoa wanajeshi wake  karibu na mpaka wake na Ukraine na kurejea katika mazungumzo yanayoongozwa kwa ushirikiano wa Ujerumani na Ufaransa.

Katika taarifa yao ya pamoja wamesisitiza umuhimu wa Urusi kuondoa wasiwasi unaosababishwa na jeshi lake katika mpaka huo na kujizuwiya na maneno ya kichokozi. 

Ujerumani na Ufaransa zasema milango ya majadliano na Urusi bado iko wazi

EU-Gipfel in Brüssel | PK Scholz und Macron
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wakizungumza na wanahabari baada ya kumalizika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels Picha: John Thys/AP Photo/picture alliance

Wamerejelea ujumbe ulioungwa mkono pia na Marekani, Uingerza na kundi la mataifa saba yaliyoinukia kiviwanda   kwamba Urusi itawajibishwa vikali ikiwemo kudhibiti ushirikiano wa taifa hilo na washirika wake iwapo itachukua hatua yoyote ya kichokozi dhidi ya Ukraine.

Siku ya Jumatatu, Umoja wa Ulaya uliiweka kampuni binafsi ya kijeshi ya Urusi Wagner Group katika orodha ya vikwazo baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo.

soma zaidi:  Mawaziri wa G7 waionya Urusi dhidi ya kuishambulia Ukraine

Hata hivyo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wamesema milango iko wazi kwa mazungumzo na Urusi, huku wakihimizwa "Mfumo wa Normandy" ambao ni mazungumzo ya pande nne yanayowajumuisha viongozi wakuu wa Ukraine, Ufaransa, Urusi na Ujerumani.

Mataifa ya Mashariki mwa Ulaya yana wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa wanajeshi wa Urusi mpakani mwa Ukraine. Rais wa Lithuania Gitanas Nauseda ambae taifa lake linapakana na Urusi ameonya kuwa hatua ya Moscow huenda ikayumbisha hali ya usalama ya eneo hilo. 

Chanzo: AFP, AP, dpa, Reuters