1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yapanga kuwa mfumo wa pamoja kushughulikia wakimbizi

17 Julai 2009

Mawaziri wa Sheria na Mambo ya ndani wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wa hapo jana mjini Stockholm Sweden, wametangaza kuunga mkono kuanzishwa utaratibu wa pamoja kushughulikia wahamiaji wanaoingia barani humo

https://p.dw.com/p/IrOk
Bendera ya EU na Sweden (rais wa eu)Picha: DW

Suala hilo la wakimbizi limekuwa mtihani mkubwa katika mshikamano ndani ya umoja huo .Nchi zote zilizoko katika eneo la bahari ya Mediterrania zinataka nchi ambazo hazina bahari kupokea wakimbizi zaidi ili kuzipunguzia mzigo.

Ni mwezi mmoja tu uliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia Roberto Maroti alipotoa wito huo kwa mawaziri wenzake wa umoja huo wa Ulaya. Na hapo jana katika mkutano wao mjini Stockholm alirejelea tena wito wake huo.

„Sheria hii katika Umoja wa Ulaya ni lazima iwekwe ya kugawana mzigo mzito wa wakimbizi wanaoingia na kutafuta hifadhi.“


Nchini Italia maelfu kwa maelfu ya wakimbizi wamekuwa wakiingia kwa kutumia usafiri wa boti wakitokea Afrika ya Kaskazini.

Hali hiyo kwa mujibu wa shirika moja la misaada ni janga kubwa. Mwaka jana zaidi ya watu elfu 70 waliingia Ulaya wakitokea Afrika kupitia bahari ya Mediterrania. Halikadhalika maelfu wamekuwa wakimiminika huko Cyprus ambako wanataabika.


Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cyprus Neoklis Sylikiotis ametaka mshikamano zaidi katika kushughulikia suala hilo.

´´Ni wakati muafaka sasa tunahitaji mshikamano zaidi kutoka kwa nchi wanachama´´


Ni katika kipindi hiki ambapo Sweden inashikilia kiti cha urais wa umoja huo, ndipo sauti za nchi hizo zilizoko katika bahari ya Mediterrania zinasikika.

Sweden yenyewe haikubaliani na kutungwa kwa sheria itakayolazimisha kuwapokea wakimbizi kutoka katika nchi wanachama zilizoko katika bahari ya Mediterrania.


Tobias Billström ni Waziri anayehusika na masuala ya uhamiaji na wakimbizi nchini Sweden.

´´Kwangu mimi kuna mambo mawili muhimu. Kwanza ni kuundwa kwa mfumo wa pamoja wa wakimbizi ikiwa na maana kuwa kuongeza zaidi mshikamano. Na pili ni suala la sheria za uhamiaji. Tunahitaji kufungua njia zaidi kwa watu ambao wataweza kuja Ulaya kufanyakazi. Tunahitaji kupanga utaratibu kwa mujibu wa mahitaji, utaratibu ambao utakuwa na faida kwa uchumi wetu na jamii yetu´´


Kwa upande wake Ujerumani nayo pia inapinga kuundwa kwa sheria ya kuwapokea wakimbizi, kwa mfano wale waliyoingia Italia au Ugiriki. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Wolfgang Schäuble amesema ni lazima kila nchi itoe msaada kutokana na uwezo wake na utayari wa kufanya hivyo. Ameunga mkono vigezo sawa katika kuwapokea wakimbizi wanaomba hifadhi.

Bundesinnenminister Wolfgang Schäuble
Waziri wa Ndani wa Ujerumani Wolfgang SchäublePicha: picture-alliance/ dpa

´´Ni suala lisilokubalika kwamba nchi moja ipokee wakimbizi hadi asilimia 90 na nyingine asilimia kumi tu, hivyo inaonesha hali haiko sawa sawa.´´


Mawaziri hao wamependekeza mfumo wa pamoja unaoitwa mpango wa miaka mitano wa Stockholm na ambao unatakiwa kupitishwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.


Mwandishi: Christoph Prößl/ Aboubakary Liongo

Mhariri: Josephat Charo