1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU na Japan zafikia makubaliano makubwa ya biashara

Caro Robi
17 Julai 2018

 Maafisa wa Umoja wa Ulaya wanatia saini makubaliano makubwa zaidi kuwahi kufikiwa kuhusu biashara huru kati ya Umoja huo na Japan, wakidhihirisha mshikamano dhidi ya Marekani ambayo inatishia biashara ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/31a3w
Brüssel EU - Japan Gipfel
Picha: picture-alliance/abaca/D. Aydemir

Maafisa wa Umoja wa Ulaya na wa Japan wamesema makubaliano hayo yanaonesha kujitolea kwao kuondoa vizuizi vya kibiashara, wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump anapoendeleza sera yake ya kuvilinda viwanda vya ndani ya nchi yake kwa kuiweka Marekani mbele.

Trump amewakera na kuwatia wasiwasi washirika wa Marekani Umoja wa Ulaya na Japan na kuwaghadhabisha washindani wake China, kwa kuongeza kodi za bidhaa zinazoingizwa Marekani, kuzitishia nchi nyingine kuwa itaziwekea vikwazo vya kibiashara na kutishia kuzua vita vya kibiashara.

Marekani yakera washirika wake

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk na Rais wa halmashauri ya umoja huo Jean Claude Junker wamewasili leo Japan, baada ya jana kufanya mazungumzo Biejing, China ambapo walitoa wito wa kuwepo utulivu badala ya mzozo katika biashara za kimataifa.

Japan Tokyo - Donald Tusk, Shinzo Abe und  Jean-Claude Juncker
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk, Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude JunkerPicha: picture-alliance/AP Imags/T. Joko

Tusk amesema ni wajibu wa pamoja kwa China, Ulaya, na pia Marekani na Urusi kutovuruga mfumo wa kimataifa wa biashara bali kuuimarisha, kutoanza vita vya kibiashara ambavyo hupelekea mizozo mikali na kuongeza bado kuna muda wa kuepusha mizozo na vurugu.

Makubaliano hayo kati ya Umoja wa Ulaya na Japan yanaunda kanda kubwa mno ya kiuchumi ambayo ni tofauti kabisa na sera ya Trump ya kulinda viwanda vya ndani ya nchi.

Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Margaritis Schinas amesema makubaliano hayo yaliyofikiwa mwezi Desemba mwaka jana, ndiyo makubaliano makubwa kabisa ya kibiashara kuwahi kufikiwa na Umoja wa Ulaya na yatafungua fursa za biashara huru zitakazojumuisha karibu thuluthi moja ya pato jumla la dunia.

EU yaimarisha miungano mipya

Umoja wa Ulaya ambao ni soko kubwa zaidi la pamoja linalohusisha nchi wanachama 28 na watu milioni 500, linajaribu kuimarisha miungano ya kibiashara na washirika wapya, tangu Trump alipoingia madarakani na kuvuruga mahusiano ya karibu ya kibiashara na mengineyo kwa kupania kuyaweka mbele maslahi ya Marekani kwanza bila kujali maslahi ya nchi nyingine.

Finnland Helsinki PK Treffen Trump Putin
Rais wa Marekani Donald Trump(Kushoto) na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/G. Dukin

Kamishna wa Umoja wa Ulaya kuhusu biashara Cecilia Malmstrom na waziri wa uchumi wa Japan Toshimitsu Motegi wamesema makubaliano hayo kati ya Japan na Umoja wa Ulaya yatatuma ishara nzito kwa ulimwengu kuwa wanakuza biashara huru dhidi ya sera ya Marekani ya kulinda viwanda vyake vya ndani.

Siku ya Jumapili, Trump aliuita Umoja wa Ulaya, maadui wa Marekani na kusisitiza Umoja wa Ulaya unajinufaisha visivyo kibiashara kutoka kwa Marekani.

Chini ya makubaliano hayo mapya, Umoja wa UIaya utafungua soko lake kwa sekta ya magari ya Japan na kwa upande wake, Japan itaziondolea kodi bidhaa za Ulaya za kilimo hasa bidhaa zitokanazo na maziwa.

Umoja wa Ulaya unatafuta kuingia katika soko la Japan linalotajwa kuwa mojawapo ya matajiri zaidi duniani, ilhali Japan inatumai kuupiga jeki uchumi wake ambao umekuwa ukipata tabu ya kupata ukuaji thabiti.

 

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri: Josephat Charo