1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU: Hali nchini Msumbiji inatia wasiwasi

16 Aprili 2020

Umoja wa Ulaya umesema unatiwa wasiwasi mkubwa na kuongezeka kwa ghasia zenye misingi ya kijihadi kaskazini mwa Msumbiji, na kuvurugika kwa hali ya kibinadamu katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/3azJV
Mosambik Montepuez - Anhänger von RENAMO verursachen Aufstände in Montepuez, Cabo Delgado
Hali ni ya wasiwasi kwenye jimbo la Cabo DelgadoPicha: DW/D. Anacleto

Katika taarifa yake ya maandishi, Umoja wa Ulaya umesema hali ya usalama katika mkoa wa Cabo Delgado ulio kaskazini mwa Msumbiji imezorota sana mnamo wiki za hivi karibuni, na kuyataja mashambulizi ambayo yamekuwa yakiongezeka.

Mkoa huo unayo miradi ya uchimbaji wa gesi yenye thamani ya mabilioni ya dola, inayoendeshwa na makampuni makubwa ya kimataifa, ikiwemo Total ya Ufaransa.

Mwezi uliopita wanamgambo waliyakamata majengo ya serikali katika mkoa huo na kupandisha bendera ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Taarifa ya Umoja wa Ulaya imesema mipango madhubuti inahitajika kuishughulikia hali ya sasa katika mkoa wa Cabo Delgado, ili kuwalinda wananchi na kufanya uchunguzi utakaohakikisha kuwa wanaohusika katika ghasia hizo wanafikishwa mahakamani.

Hali hiyo ya vurugu, umesema Umoja wa Ulaya, imesababisha dadi kubwa ya wakaazi kuzihama nyumba zao.

Hali ni mbaya kwenye jimbo la Cabo Delgado

Mosambik Illegale Edelstein-Minen
Picha: DW/E. Valoy

Kwa mujibu wa Askofu wa Dayosisi ya Pema, Dom Luiz Fernando Lisboa, tayari watu 200,000 wameyakimbia makaazi yao kutokana na ghasia hizo, nalo shirika la Madaktari wasio na Mpaka, MSF linasema wengine 700 wamepoteza maisha.

Aidha, Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Msumbiji kuchunguza haraka kisa cha kutoweka mwandishi wa habari wa redio ya kijamii ya Palma wiki iliyopita. Mwandishi huyo, Abu Mbaruko alitoweka alipokuwa njia akirejea nyumbani kutoka kazini, na hadi sasa hajulikani alipo.

Tarehe saba Aprili Abu Mbaruko aliwatumia wenzake ujumbe wa maandishi akiwaarifu kuwa alikuwa amezingirwa na wanajeshi, na tangu hapo, hii ikiwa ni kwa mujibu wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika-MISA, mwandishi huyo hajaweza kupokea simu anazopigiwa.

Umoja wa Ulaya kuisaidia Msumbiji 

Mosambik Maputo | Einweihungszeremonie Filipe Nyusi, neuer Präsident
Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji Picha: Reuters/G. Lee Neuenburg

Licha ya ahadi iliyotolewa na rais wa Msumbiji Filipe Nyusi, vyombo vya usalama vya Msumbiji vinavyosaidiwa na mashirika binafsi ya usalama ya kimataifa, havijaweza kuyasimimasha mashambulizi mkoano Cabo Delgado.

Umoja wa Ulaya katika taarifa yake umeahidi kuisaidia Msumbiji katika juhudi zake za kuyasambaratisha makundi yanayovuruga usalama.

Hata hivyo, kamanda mkuu wa polisi ya Msumbiji Bernardino Rafael amekanusha habari za makundi hayo kuyadhibiti maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji, akisema kilichopo na mashambulizi madogo ya wahalifu katika baadhi ya sehemu.

Kamanda huyo lakini amekiri kuwa hali ya hofu imetanda katika baadhi ya maeneo ya mbali na miradi ya kuchimba gesi, kama vile Mocimboa da Praia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga