1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan ataka Uturuki isusie bidhaa za Marekani

Yusra Buwayhid
14 Agosti 2018

Sarafu ya Uturuki ya lira iliyokuwa imeanguka thamani wiki iliyopita, imeimarika kidogo Jumanne katika masoko ya hisa, huku Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akitoa wito wa kususia bidhaa za elktroniki za Marekani.

https://p.dw.com/p/33892
Türkei Lira Banknoten
Picha: Reuters/M. Sezer

 

Hapo jana lira 6.9 ilikuwa sawa na dola moja ya Kimarekani. Sarafu hiyo ya Uturuki imeanguka kwa asilimia 45 mwaka huu, kutokana na wito wa Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdogan wa kutaka kuwepo riba ya kiwango cha chini pamoja na kuharibika kwa uhusiano wake na Marekani. 

Hata hivyo, sarafu ya lira imeimarika kidogo Jumanne kufuatia hatua kadhaa za benki kuu za kuimarisha ukwasi, pamoja na kutolewa taarifa kwamba waziri wa fedha wa Uturuki amepanga kuzungumza kwa njia ya simu na wawekezaji ili kuwapunguzia wasiwasi.

Wafanyabiashara wamesema mpango wa Waziri wa Fedha Berat Albayrak wa kuzungumza na wawekezaji wapatao 1,000 kwa njia ya simu, kujadili suala la uchumi wa Uturuki, utasaidia kufufua thamani ya sarafu hiyo ya lira.

"Wasiwasi bado unaendelea kuwepo katika soko lakini naweza kusema kuna matumaini kidogo kwa mara ya kwanza kwa muda mrefu," amesema mfanyabiashara mmoja wa fedha za kigeni.

Wafanyabiashara wa kawaida nchini Uturuki tayari wameshaanza kuathirika na mgogoro huo wa sarafu ya lira.

"Bidhaa nyingi tunazouza zinatoka nje ya nchi, pamoja na malighafi. Tuna bidhaa nyingi ambazo zinatoka nje ya nchi, ambazo pia zinauzwa kwa fedha za kigeni, kutoka Ulaya na Marekani, ndiyo maaan tunaathirika moja kwa moja na vibaya sana," amesema Sukru Gumus, mmiliki duka la vitu vya rejareja.

Türkei Ankara Rede Erdogan
Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan katika mkutano na wanadiplomasia, Ikulu ya Rais mjini Ankara, UturukiPicha: picture-alliance/Xinhua/Turkish Presidential Palace

Uturuki kususia bidhaa za kielktroniki za Marekani

Wakati huo huo, Rais Erdogan ametoa wito Jumanne wa kususia bidhaa za elektroniki za Marekani, ambayo imeiwekea Uturuki vikwazo vya kibiashara pamoja na kuipandishia ushuru wa bidhaa.

Erdogan amesema Uturuki imechukua hatua muhimu kuhusu uchumi, katikati ya mgogoro unaoikabili sarafu yake ya lira uliochochewa na Marekani. Erdogan ameongeza kwamba ni muhimu kuwa na msimamo thabiti wa kisiasa, na Uturuki haitotumia fedha ya kigeni kwani hilo litamaanisha kukubali kushindwa na adui wake.

Uhusiano kati ya Uturuki na Marekani umeharibika kutokana na masuala kadhaa yaliosababisha mkwaruzano kati yao. Miongoni mwao ni pamoja na hatua ya Uturuki kuingilia kati vita vya Syria, mpango wa Uturuki wa kutaka kununua mifumo ya ulinzi kutoka Urusi, pamoja na kuwekwa kizuizini nchini Uturuki mchungaji wa Kimarekani, Andrew Brunson.

Kwa upande wa Ujerumani, kansela Angela Merkel Jumatatu aliisisitiza Uturuki kufanya kila iwezalo kuhakikisha uhuru wa benki kuu, huku viongozi wengine wa ngazi za juu wa Ujerumani wakiwa na wasiwasi kutokana na matatizo ya kiuchumi ya Uturuki.

Merkel amesema Ujerumani ingependa kuiona Uturuki ikiimarika kiuchumi, na sio tu kwa maslahi ya nchi hiyo bali pia kwa maslahi ya Ujerumani.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ap

Mhariri: Josephat Charo