1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan aondoa pingamizi kwa Sweden kujiunga na NATO

11 Julai 2023

Rais wa Uturuki amekubali kuunga mkono ombi la Sweden kuwa mwanachama wa Jumuiya ya kujihami NATO, na atawasilisha uamuzi huo haraka iwezekanavyo ili upasishwe na Bunge la Ankara.

https://p.dw.com/p/4ThV4
Natogipfel in Litauen Eingung zwischen Erdogan und Ulf Kristersson
Picha: Henrik Montgomery/ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Hayo yameelezwa jana usiku na Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ambaye alikutana kwa mazungumzo na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Waziri Mkuu wa Sweden Ulf Kristersson huko Vilnus, Lithuania kunakoanza hii leo mkutano wa kilele wa siku mbili wa NATO.

Hata hivyo, taarifa ya pamoja iliyotolewa na viongozi hao watatu haijabaini ni kwa muda gani Bunge la Uturuki linalazimika kuidhinisha ombi hilo la Sweden.

Stoltenberg amesema kukamilisha ombi la Sweden ni hatua ya kihistoria inayonufaisha usalama wa washirika wote wa NATO hasa katika wakati huu muhimu.

Soma pia: Erdogan aweka sharti jipya kwa Sweden kujiunga na NATO

 

Biden kukutana na Zelensky huko Vilnius

G7 Gipfel in Japan, Hiroshima | Joe Biden mit Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy katika mkutano wa G7 huko Japan (21.05.2023)Picha: Susan Walsh/POOL/AFP/Getty Images

Rais wa Marekani Joe Biden atakutana hapo kesho kwa mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy katika mji mkuu wa Lithuania, ambako viongozi wa NATO wamekusanyika katika mkutano wa kilele ambao utatawaliwa na ajenda ya vita nchini Ukraine pamoja na shinikizo la Kyiv la kutaka ikaribishwe haraka ndani ya jumuiya hiyo.

Nchi wanachama wa NATO wanajadili jinsi ya kuondokana na mgawanyiko kuhusu jitihada za Ukraine kuelekea uanachama lakini wanadiplomasia wengi wamebaini kuwa tofauti hizo zimepungua baada ya walio wengi kuafiki kuwa Ukraine haiwezi kujiunga na NATO wakati huu wa vita.

Soma pia:Ukraine:Tumerejesha maeneo yaliodhibitiwa na Urusi 

Wanachama wa NATO katika Ulaya Mashariki wameunga mkono msimamo wa Kyiv, wakibaini kwamba, kuijumuisha Ukraine chini ya mwamvuli wa usalama wa pamoja wa NATO ndio njia bora ya kuzuia Urusi kuishambulia tena.

Mwaka mmoja tangu Urusi kuivamia Ukraine