1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Enzi inayomalizika na inayokuja Marekani

Oumilkheir Hamidou
12 Januari 2017

Urithi wa Barack Obama na mustakbali wa Marekani ndio mada zilizohanikiza magazetini huku enzi za Obama zikikurubia kumalizika na atakayekamata nafasi yake kama rais wa Marekani, Donald Trump, akizidi kuonyesha misuli.

https://p.dw.com/p/2VgSi
New York City Trump erste PK als designierter Präsident
Picha: Getty Images/AFP/T. A. Clary

Mada kuhusu kupungua sana idadi ya wanaoingia Ujerumani kuomba kinga ya ukimbizi, nayo pia imegonga vichwa vya habari. Tunaanzia lakini Marekani ambako wahariri wa magazeti ya Ujerumani sio tu wameichambua hotuba ya kuaga iliyotolewa na Barack Obama mjini Chicago, bali pia mkutano wa kwanza na waandishi habari wa rais mteule Donald Trump. Gazeti la mjini Cologne,"Stadt-Anzeiger linaandika: "Yeyote yule aliyejiwekea matumaini pengine mfanya kampeni ya  matusi na vitisho Donald Trump angebadilika na kuwa kiongozi wa kuheshimika, anabidi asahau. Trump ni Trump. Habadiliki anaendelea na mtindo wake hata kama ni wa kuchusha."

Kwanini hawakuwa na mgombea ambadala wa Hillary Clinton?

Gazeti la Rhein-Zeitung linahisi Barack Obama anabeba pia sehemu ya makosa kuona urithi wake unavurugwa. Gazeti hilo la mjini Koblenz linahisi Obama angemtafuta mapema mrithi mbadala kwa Hillary Clinton kama mgombea wa wadhifa wa rais kutoka chama chake. Kuanzia january 20 inaanza enzi ya  Trump. Enzi hiyo ni hatari kubwa kabisa kwa urithi wa Obama. Kwasababu Trump anawekewa matumaini  tangu na makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia  mpaka na yale ya wabaguzi. Na makundi yote hayo yamekuwa kwa miaka kadhaa  sasa yakiandaa mikakati ya kuipindua siasa ya Obama. Kilichosalia ni matumaini tu kwamba Trump atawalenga wale ambao kwa wingi wao wamempigia kura: wale walioachwa kando na mfumo wa utandawazi. Na hao hao wangekuwa wale ambao Obama angewapigania, kama rais wa Marekani.

Marekani iendelee kuwa ya kiliberali na waazi kwa dunia

Gazeti la "Nürnberger Zeitung" linasema hata kama enzi ya Obama haijatakata hivyo, wengi wanamlilia."Kwamba kiongozi mwenye haiba, kipaji na nuru nafasi yake inashikiliwa na muimla mwenye hasira, hilo linamkera sana Obama. Ni sawa kwake anapopania kuutetea urithi wake ( ambao Trump anapanga kuufuta mara baada ya kuingia madarakani) na hasa anapopigania kuendelezwa demokrasia nchini mwake. Ndio maana Obama ameitumia hotuba yake ya kuaga kutoa nasaha Marekani iwe ya kiliberali na wazi kwa dunia."

Idadi ya wakimbizi imepungua sana Ujerumani

Mbali na mada hiyo kuhusu Marekani, wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha pia na kupungua idadi ya wahamiaji wanaoingia humu nchini. Gazeti la Saabrücker Zeitung linatoa sababu ya hali hiyo na kuandika: "Idadi hiyo inaficha sababu iliyopelekea kuwa hivyo. Cha kutajwa kwanza ni idadi ya wale waliokwama katika njia ya Balkan. Kwamba kundi hilo linalokadirika halikuweza kupatiwa ufumbuzi wa kiutu ni aibu kwa Ulaya na pia kwa sera za Ujeruman kuelekea wakimbizi ambazo hadi wakati huu zilikuwa zikisifiwa. Makubaliano pamoja na Uturuki yayonatajwa kuwa sababu ya kupungua idadi ya wahamiaji, yanatajwa na gazeti la Saarbrücker Zeitung kugeuka kua makubaliano pamoja na shetani  kwa wakati wote ambapo Erdogan anazidi kugeuka muimla.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef