Enrique apuuzia maswali kuhusu hatma yake na Barcelona
22 Mei 2015Hayo ni wakati vigogo hivyo vya Katalunia vinaweza kunyakua mataji matatu msimu huu. Akifikia mwisho wa msimu wake wa kwanza akiifunza timu hiyo ya Camp Nou , Luis Enrique ana mkataba hadi Juni 2016 lakini klabu hiyo inatarajia kufanya uchaguzi wake wa rais katikati ya mwaka huu na utawala mpya ina maana huenda ukaamua kuleta sura mpya.
Nae kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti amekiri kwamba bado hajafahamu iwapo ataendelea kuwa kocha wa klabu hiyo msimu ujao. Real Madrid inamaliza kampeni ya msimu huu kwa kupambana na Getafe leo Jumamosi, lakini itafanya hivyo bila taji lolote kubwa baada ya Barcelona kukamilisha ubingwa wake wa 23 katika La Liga wiki iliyopita. Ancelotti amesema hajazungumza na uongozi wa klabu hiyo , na wala uongozi haujazungumza nae. Lakini ameongeza Jumapili ama Jumatatu watakutana na kuzungumza juu ya hatima yake na ya klabu.
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew amesema mabingwa hao wa dunia wanapanga kuwanyanyua wachezaji chipukizi chini ya miaka 21 na kuwaingiza katika kikosi chake cha timu ya taifa katika pambano la kirafiki na Marekani na kisha mpambano wa kuwania tikiti ya kucheza katika michuano ya mataifa ya bara la Ulaya dhidi ya Gibraltar. Juni 10 Ujerumani itakuwa wenyeji wa kocha Juergen Klinsmann na kikosi chake cha US Boys mjini Kolon, na kisha watacheza na kisha kucheza na Gibraltar siku tatu baadaye mjini Faro , Ureno.
Kocha wa Liverpool Brendan Rodgers anatarajia kuwa mchezaji wake muhimu wa kiungo Raheem Sterling kutumikia timu hiyo hadi utakapomalizika mkataba wake ambapo imebakia miaka miwili licha ya madai yanayotolewa na wakala wa mchezaji huyo kwamba hatakubali mkataba mwingine na timu hiyo.
Mustakabali wa Raheem umekuwa suala la majadiliano makali katika vyombo vya habari tangu alipozuwia mazungumzo kwa ajili ya mkataba mpya na wakala wake Aidy Ward akisema wiki hii kwamba kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 hatarefusha mkataba wake hata kama atapatiwa pendekezo la mshahara wa pauni laki tisa kwa wiki.
Liverpool ilivunja mkutano na Sterling siku ya Ijumaa kujadili hali yake ya baadaye kufuatia matamshi ya ward , lakini Rodgers anatarajia mazungumzo yataanza tena baada ya mchezo wa mwisho wa msimu dhidi ya Stoke City.
Mwandishi: Sekione Kitojo
Mhariri: Mohammed Khelef