Emirati yapinga kuhamishwa kwa Wapalestina Gaza
19 Februari 2025Haya yanafanyika wakati ambapo Israel imewafungulia mashtaka wanajeshi 5 kwa kumtesa mfungwa wa Kipalestina.
Rais wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan Jumatano alikutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio huko Abu Dhabi, na kulingana na shirika la habari la Emirati WAM, rais huyo aliweka wazi kwa Rubio kwamba ni muhimu kuhusisha ujenzi mpya wa Gaza na mkondo utakaopelekea amani ya kudumu itakayotokana na suluhisho la mataifa mawili.
Wanajeshi wa Israel wafunguliwa mashtaka
Msimamo wa Falme za Kiarabu katika mzozo wa Israel na Palestina ni muhimu kwasababu ni mojawapo ya mataifa 4 ya Kiarabu yaliyosawazisha mahusiano yake na Israel wakati wa utawala wa kwanza wa Trump na ni nchi iliyokuwa na dhima katika ufadhili wa kazi za ujenzi baada ya mizozo iliyopita Gaza.
Matamshi ya Sheikh Zayed yanakuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kupendekeza Marekani kuichukua Gaza na kuwahamisha Wapalestina na kuwapeleka Jordan na Misri.
Naye rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi Jumatano aliitaka jamii ya kimataifa kubuni mpango wa kuijenga upya Gaza iliyoharibiwa vibaya na vita, bila kuwahamisha Wapalestina.
Wakati huo huo, kiongozi wa mashtaka katika jeshi la Israel amewafungulia mashtaka wanajeshi 5 wanaoshukiwa kujihusisha na kumtesa mfungwa mmoja wa Kipalestina.
Kulingana na jeshi la Israel, wanajeshi hao wanadaiwa kumtesa mfungwa huyo na hata kumdhalilisha kingono. Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa wanajeshi hao walimtesa mwanachama huyo wa kundi la wanamgambo la Hamas, kiasi cha kuwa alilazimika kukimbizwa hospitali kwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata.
Awali jeshi la polisi la Israel lilikuwa limewakamata wanajeshi 10 waliohusishwa na kisa hicho ila watano kati yao waliachiwa huru baadae.
Mazungumzo ya pili ya amani ni magumu zaidi
Hayo yakiarifiwa, afisa mmoja wa Israel amesema kuwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amemteua mwandani wake kuongoza mazungumzo ya kusitisha mapigano ya awamu ya pili na wanamgambo wa Hamas.
Ron Dermer ambaye ni mzaliwa wa Marekani, ni waziri ambaye anachukuliwa kama mshauri wa karibu sana wa Netanyahu. Aliwahi kuhudumu kama balozi wa Israel nchini Marekani na ni mwanaharakati wa zamani wa chama cha Republican aliye na mahusiano ya karibu na Rais Donald Trump.
Israel na Hamas bado hawajafanya majadiliano ya pili ya usitishwaji mapigano ambayo ni magumu zaidi, huku awamu ya kwanza ya mazungumzo ikiwa itaisha mwanzoni mwa mwezi Machi.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Ulimwenguni WHO, limesema kuwa kampeni kubwa ya utoaji chanjo ya polio kwa watoto huko Gaza, itaanza tena siku ya Jumamosi.
Katika taarifa Shirika hilo limesema linawalenga zaidi ya watoto nusu milioni katika zoezi hilo la utoaji chanjo, kwani mazingira ya sasa huko Gaza yanapelekea kusambaa pakubwa kwa virusi vya polio.
Vyanzo: DPA/AP/Reuters