1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Riyadh yaitisha mkutano wa kilele kuhusu ujenzi wa Gaza

17 Februari 2025

Pendekezo tata la rais Donald Trump la kutaka kuwahamisha Wapalestina kutoka ardhi yao ya Gaza lachochea juhudi kabambe za mataifa ya Kiarabu za kuitetea ardhi hiyo.

https://p.dw.com/p/4qb9W
 Waziri wa mambo ya kigeni wa Saudi Arabia,Mwanamfalme Faisal bin Farhan bin Abdullah
Mwanamfalme Faisal bin Farhan bin AbdullahPicha: Saudi Press Agency/APA/ZUMA/picture alliance

Mjadala unashika kasi kuhusu suala la ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza.

Saudi Arabia inajiandaa kuwakaribisha viongozi wa ngazi za juu katika mkutano wa kilele utakaowaleta pamoja viongozi kutoka mataifa mbali mbali ya ulimwengu wa Kiarabu.

Viongozi kutoka Misri,Jordan na mataifa ya Ghuba wanatarajiwa mjini Riyadh siku ya Ijumaa kulijadili suala la ujenzi mpya wa Gaza iliyoharibiwa kabisa kwa vita.

Vyanzo vya kidiplomasia kutoka mataifa ya Kiarabu vimedokeza hayo kwa shirika la habari la kijerumani Dpa ambapo, imeelezwa kwamba mkutano huo utajikita kwenye pendekezo lililowekwa mezani na Misri la kutaka Gaza ijengwe upya chini ya usimamizi kamili wa mataifa ya Kiarabu.

Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas
Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas Picha: Saudi Press Agency/Newscom/picture alliance

Mivutano imekuwa ikiongezeka baada ya pendekezo la utata la rais wa Marekani Donald Trump la kutaka kuwahamisha kabisa Wapalestina kiasi milioni mbili wakaazi wa kutoka Gaza na kuwapeleka kwenye mataifa mengine jirani ya kiarabu.

Mpango wa Misri uliopo mezani

Wazo hilo bila shaka limepingwa vikali na Misri,Joradn na mataifa mengine yenye nguvu katika ukanda huo, wakiliona kama pendekezo linalokiuka mamlaka na mipaka ya Wapalestina.

Na kutokana na hilo,Misri imeamuwa kuanzisha juhudi mahususi za kuweka mezani mpango wake ili kuizuia Marekani na Israel kushinikiza ajenda yao ya kutaka kuwaondosha Wapalestina kwenye ardhi yao ya Gaza.

Makadirio ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa yanaonesha kwamba ujenzi mpya wa Gaza huenda ukahitaji kiasi dola bilioni 53 huku dola bilioni 20 zikihitajika katika awamu ya mwanzo ya miaka mitatu ya ujenzi huo.

Mfalme  Abdullah II , Abdel Fattah El-Sisi na Mahmud Abbas
Mfalme Abdullah II , Abdel Fattah El-Sisi na Mahmud AbbasPicha: Palestinian Presidency/AA/picture alliance

Wakati viongozi wa mataifa ya Kiarabu na Ghuba wakijiandaa kukutana Riyadh Ijumaa, hivi leo Jumatatu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amekutana na mwenzake wa Saudi Arabia mwanamfalme Faisal bin Farhan mjini Riyadh.

Ziara hiyo ya Marco Rubio Riyadh imefuatia ziara yake Israel ambako alikuwa na mazungumzo na waziri mkuu Benjamin Netanyahu yaliyojikita juu ya pendekezo hilo la rais Trump la kuwahamisha Wapalestina wa Gaza kwenye mataifa ya Kiarabu.

Msimamo wa EU kuhusu Gaza

Pendekezo hilo la Trump sio tu limekataliwa na viongozi wa mataifa ya Kiarabu, hata mjini Brussels viongozi wa Umoja wa Ulaya hawakubaliani na mtazamo wa Marekani.

Umoja huo nyaraka zilizoonekana na shirika la habari la Reuters hii leo zinaonesha viongozi wa Umoja huo wanapanga wiki ijayo kuiambia Israel kwamba Wapalestina waliopoteza makaazi yao kwenye vita wanapaswa kuhakikishiwa kurudi kwenye makaazi yao kwa heshima na Umoja huo uko tayari kuchangia katika ujenzi mpya wa Gaza.Soma Pia: Ziara ya Rubio: Netanyahu asifu msimamo wa Trump kuhusu Gaza

Umoja wa Ulaya unapanga kuuweka wazi msimamo wake huo mbele ya Israel Februari 24 katika kikao kati ya Jumuiya hiyo na baraza la Israel.

Pamoja na hayo, imeripotiwa leo kwamba Jeshi la Israel limesema limemuua kamanda wa operesheni za kundi la Hamas katika shambulio la anga kusini mwa Lebanon,ikituhumu Mohammed Shahin, alikuwa akipanga kufanya mashambulio dhidi ya Israel kutokea ardhi ya Lebanon.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yamefanyika mkesha wa siku ya mwisho ya muda uliowekwa wa makubaliano tete kati ya Israel na Hezbollah.

Vifaru vya kijeshi vya Israel, Kusini mwa Lebanon
Vifaru vya kijeshi vya Israel, Kusini mwa Lebanon Picha: Stringer/Anadolu/picture alliance

Rais Joseph Aoun ametowa mwito wa wasimamizi wa makubaliano hayo kuishiniza Israel iondowe wanajeshi wake katika ardhi ya Lebanon kufikia Jumanne.

Ndani ya Israel kwenyewe,familia na jamaa  za waliotekwa nyara na Hamas,wamefanya maandamano leo Jumatatu kuadhimisha siku 500 za kutekwa kwa wapendwa wao. Jumla ya Waisraeli 73 bado wanashikiliwa katika Ukanda wa Gaza, 36 kati yao inasadikika hawako hai.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW