1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yasema LA, kwa pendekezo la utawala wa kijeshi Niger

22 Agosti 2023

ECOWAS yakataa pendekezo la utawala wa kijeshi nchini Niger kuunda serikali ya mpito kisha kuaandaa uchaguzi katika muda wa miaka mitatu ijayo.

https://p.dw.com/p/4VQUB
ECOWAS tayari imetishia kuwa itatuma jeshi nchini Niger iwapo juhudi za kidiplomasia zitashindwa kuwashawishi wanajeshi kuachia madaraka.
ECOWAS tayari imetishia kuwa itatuma jeshi nchini Niger iwapo juhudi za kidiplomasia zitashindwa kuwashawishi wanajeshi kuachia madaraka.Picha: Gerard Nartey/AFP/Getty Images

Kamishna wa Jumuiya ya ECOWAS Abdel-Fatau Musah amesema msimamo wa taasisi hiyo ya kikanda wa kuwataka majenerali walioipindua serikali waondoke madarakani bado haujabadilika.

Amesema matakwa ya ECOWAS ya kuachiwa bila masharti kwa rais Mohammed Bazoum na kurejeshwa utawala wa katiba haraka iwezekenavyo bado hayajaondolewa. 

Jumuiya hiyo imerejea msimamo huo baada ya kiongozi wa kijeshi wa Niger Jenerali Abdourahamane Tiani kusema siku ya Jumamosi kuwa wanalenga kubakia madarakani kwa miaka mitatu kabla ya kurejea kwa utawala wa kiraia.

Pia alisema jeshi liko tayari kwa mazungumzo kuhusu mzozo unaoligubika taifa hilo tangu walipochukua madaraka mnamo Julai 26.