1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yafunga mipaka yake na Mali

10 Januari 2022

Mataifa ya Afrika Magharibi yamekubaliana kuiwekea Mali vikwazo vikali ikiwemo kufunga mipaka yao, kuvunja mahusiano ya kidiplomasia na kuweka vikwazo vikali vya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/45KYX
Ghana Accra | Economic Community of West African States | ECOWAS
Picha: IVORY COAST PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Vikwazo hivyo vipya kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi – ECOWAS yenye nchi 15 wanachama vinaonyesha jinsi ilivyoufanya msimamo wake kuwa mgumu kuelekea Mali, ambayo viongozi wa mpito wamependekeza kuandaa uchaguzi Desemba 2025 badala ya Februari mwaka huu kama walivyokubaliana awali na jumuiya hiyo.

Soma pia: Mpango wa kuchelewesha uchaguzi wapingwa Mali

Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wao wa dharura mjini Accra, Ghana, ECOWAS imesema hatua ya serikali ya kijeshi kuchelewesha utaratibu wa kurejesha utawala wa kiraia haikubaliki kamwe. Jean-Claude Kassi Brou ni Rais wa Halmashauri Kuu ya ECOWAS "Hii ina maana kuwa serikali haramu ya mpito ya kijeshi itawashikilia mateka watu wa Mali kwa miaka mitano ijayo. Jumuiya hii inasisitiza wito wake kwa viongozi wa mpito kuzingatia shughuli zinazolenga kurejea kwa haraka kwa utaratibu wa kikatiba."

Ghana Accra | Economic Community of West African States | ECOWAS
Viongozi wa ECOWAS walikutana Accra Picha: IVORY COAST PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Jumuiya hiyo imesema imekubaliana kuweka mara moja vikwazo vipya vya ziada. Ni pamoja na kufungwa mipaka ya ardhini na angani ya wanachama wake na Mali, kusitishwa kwa miamala isiyo ya lazima ya kifedha, kufungia mali za serikali ya Mali katika benki za kibiashara za ECOWAS na kuwaita mabalozi wao kutoka Bamako. Wakati huo huo, Chama cha Kichumi na Kifedha cha Afrika Magharibi UEMOA kimeziagiza taasisi zote za kifedha chini ya mwamvuli wake kusitisha uwanachama wa Mali mara moja, na kuzuia nchi hiyo kujihusisha na masoko ya kifedha ya kikanda. Roch Kabore ni Rais wa Burkina Faso "Hata kama tunafahamu hali ilivyo ngumu nchini humo, tunafikiri kuwa mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayolenga kuibadilisha Mali yanaweza tu kuongozwa na serikali iliyochaguliwa kidemokrasia."

Serikali ya mpito ya Mali imesema imeshangazwa na maamuzi hayo. Katika jibu lake, imeapa kuufunga upande wake wa mpaka na mataifa wanachama wa ECOWAS, kuwaita mabalozi wake, na kubakia na haki ya kufikiria upya uwanachama wake katika jumuiya hiyo.

Soma pia: Mali yakanusha uwepo wa mamluki wa Urusi

Msemaji wa serikali hiyo Abdoulaye Maiga amesema mapema leo kwenye televisheni kuwa serikali inalaani vikali vikwazo hivyo ilivyosema ni haramu na visivyo halali na kuwahimiza Wamali kuwa watulivu.

Awali walisema uchaguzi unacheleweshwa kwa sehemu kwa sababu ya changamoto ya kuandaa zoezi la kidemokrasia katikati ya uasi mkali wa itikadi kali.

AFP/Reuters